1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya RSF vyawaua wanakijiji 28 na kujeruhi wengine 280

8 Aprili 2024

Vikosi vya kijeshi vya Sudan vimewauwa takriban watu 28 katika shambulio lililofanyika kwenye kijiji kimoja kusini mwa Khartoum mwishoni mwa juma, madaktari wamesema mauaji hayo yametokea katika kijiji cha Um Adam

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Kiogozi wa kundi la wanamgambo wa RSF Mohamed Hamdan DagloPicha: Ashraf Shazly/AFP

Vikosi vya kijeshi vya Sudan vimewauwa takriban watu 28 katika shambulio lililofanyika kwenye kijiji kimoja kusini mwa mji mkuu Khartoum mwishoni mwa juma, Kwa mujibu ripoti ya kamati ya madaktari katika eneo hilo ni kwamba kikosi cha wanamgambo wa RSF kilifanya mauaji hayo katika kijiji cha  Um Adam, karibu kilomita 150 kutoka mjini Khartoum.

Soma zaidi. WFP yafikisha msaada wa chakula Darfur

Vita nchini Sudan kati ya jeshi la Sudan lililopo chini ya Jenerali  Abdel Fattah al-Burhan, na aliyekuwa makamu wake wa zamani na kiongozi wa kundi la wanamgambo wa RSF Mohamed Hamdan Daglo vinaendelea kuchukua sura mpya kila uchao tangu kuzuka kwake April 15 mwaka uliopita.

Wanamgambo wa RSF wakiwa na kiongozi wao Mohamed Hamdan DagloPicha: Rapid Support Forces/AFP

Kwa mujibu wa wataalam wa Umoja wa Mataifa, maelfu ya watu wameuawa, wataalam hao wanatoa makadirio yanayoonyesha kuwa karibu watu 15,000 wameuawa katika mji wa Darfur pekee.

Shambulizi la Jumamosi limewaua 28

Shambulizi la Jumamosi limewauwa watu 28 katika kijiji cha Um Adam na zaidi ya watu wengine 280 walijeruhiwa, taarifa ya kamati ya madaktari imesema.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa ipo idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha na kujeruhiwa  kijijini humo ambao hawakuweza kuwahesabu kutokana na vita vinavyoedelea na ugumu wa kufikia vituo vya afya.

Soma zaidi. Watu 12 wauawa katika shambulizi la droni nchini Sudan

Baada ya shambulio hilo, taarifa ya kamati ya wanaharakati  wa eneo hilo ilikuwa imetoa idadi ya watu 25 kuwa ndio waliopoteza maisha ingawa kwa sasa kamati ya madaktari imesema idadi hiyo imeongezeka na kuwa 28.

Raia wa Sudan wakiwa wanapatiwa msaada wa huduma ya kwanza katika hospitali ya Adre, mjini DarfurPicha: Mohammad Ghannam/MSF/REUTERS

Chanzo katika Hospitali ya Manaqil iliyoko umbali wa kilomita 80 kimethibitisha kwa shirika la habari la AFP kuwa wamepokea majeruhi 200 wa shambulio hilo huku baadhi yao wakifika wakiwa wamechelewa.

Hospitali hiyo imeongeza kuwa inakabiliwa na uhaba mkubw awa damu na haia wafanyakayzi wa kutosha kuweza kuwahudumia wagonjwa wanaofika hospitalini humo.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya vituo vya afya vya Sudan havifanyi kazi na vilivyosalia vinapokea wagojwa wengi zaidi ya uwezo wao.

Soma zaidi. Baraza la usalama lahimizwa lisaidie msaada upelekwe Sudan

Pande zote mbili katika mzozo huo zimekuwa zikishutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia, uvamizi wa kutumia makombora katika maeneo ya makazi,  uporaji na kuzuia misaada.

Zaidi ya wasudan 550,000 wameyakimbia makazi yao nchini Sudan kufuatia vita vinavyoendelea nchini humoPicha: LUIS TATO/AFP

Tangu kuchukua jimbo la Al-Jazira kusini mwa Khartoum mwezi Desemba, RSF imezingira na kushambulia vijiji vizima kama vile Um Adam.

Kufikia mwezi Machi, Karibu vijiji na makazi 108 kote nchini Sudan vilikuwa vimechomwa moto na kuharibiwa kwa kiasi kikubwa. Shirika la kufichua ukiukaji wa Haki za binadamu mtandaoni CIR chenye makao nchini Uingereza kimebaini.

Vita hivyo pia vimeharibu zaidi ya makazi ya watu milioni 8.5, kuharibika kwa miundombinu na kuidumbukiza nchini hiyo kwenye baa la njaa.