1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Sudan Kusini vimewasili DRC

3 Aprili 2023

Wanajeshi wa Sudan Kusini waliwasili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumapili ili kujiunga na jeshi la kikanda katika eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23.

DRK Truppen aus dem Südsudan landen in Goma
Picha: Glody Murhabazi/AFP

Kuwasili kwao kumesadifiana na taarifa zilizotolewa na wakazi, viongozi na maafisa wa afya za kuuliwa kwa watu 14 kwenye mashambulizi tofauti katika mkoa wa Kivu Kaskazini mwishoni mwa juma katika mazingira ambayo bado hayajafahamika.

SOMA PIA; Waasi wa M23 wapuuza wito wa Viongozi wa EAC

Kulingana na taarifa ya shirika la habari la AFP takriban wanajeshi 45 waliwasili katika mji wa Goma majira ya asubuhi, huku wanajeshi wengine wakitarajiwa kuwasili katika siku zijazo.

Wanajeshi hao wa Sudan Kusini ni sehemu ya jeshi la nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambalo liliundwa mwezi Juni mwaka jana ili kuleta utulivu mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ambako sehemu kubwa ya eneo hilo inakabiliwa na makumi ya makundi yenye silaha, urithi wa vita vya kikanda ambavyo vilipamba moto katika miaka ya 1990 na 2000.

SOMA PIA; DRC: Mauaji dhidi ya raia yanaendelea licha ya uwepo wa vikosi vya usalama

Kanali Jok Akech, afisa wa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki alikikaribisha kikosi kutoka Sudan Kusini.

Hata hivyo haijabainika kikosi cha Sudan Kusini kitakuwa na ukubwa gani, wala kitapelekwa wapi, lakini mwezi Disemba Sudan Kusini ilisema kwamba itatuma wanajeshi 750 nchini Kongo.

Kujulikana kwa M23

Picha: Guerchom Ndebo/AFP

M23 ilianza kujulikana kimataifa mwaka wa 2012 ilipoiteka Goma, kabla ya kukabiliwa na hatimaye kutoweka. Lakini kundi hilo linaloongozwa na Watutsi liliibuka tena mwishoni mwa mwaka 2021, likisema kuwa serikali ilipuuza ahadi ya kuwajumuisha wapiganaji wake katika jeshi.

Juhudi mbalimbali za kikanda zilizokusudiwa kusuluhisha mzozo huo hazijafanikiwa ikiwa ni pamoja na makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyoongozwa na Angola ambayo yalitarajiwa kuanza Machi 7 lakini yalisambaratika.

Kulingana na ratiba iliyochapishwa katikati mwa Februari na Jumuiya ya Kikanda, Machi 30 ilipaswa kuwa mwisho wa kujiondoa kwa makundi yote yenye silaha, lakini tarehe hiyo haikuheshimiwa.

Kamanda wa kikosi cha EAC, Jenerali wa Kenya Jeff Nyagah, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba mpango wa kujiondoa kwa M23 utakwenda kwa hatua.

Msemaji wa kikosi kipya cha Uganda Kapteni Kato Ahmad Hassan amesema kwamba wanajeshi wa Uganda watakuwa "kikosi kisichoegemea upande wowote na hakitapigana na M23".

Kundi la waasi la M23 linasalia kutawala maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini, na  linakaribia kuuzingira mji wa Goma.

SOMA PIA; Kongo yaomba msaada wa dola bilioni 2.25 za msaada wa kiutu

Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23, jambo ambalo Marekani, nchi nyingine kadhaa za Magharibi na wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa wanakubaliana nalo, lakini Kigali inakanusha.

AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW