Vikosi vya Syria vyaendeleza mashambulizi dhidi ya wapinzani
16 Februari 2012Watu wasiopungua wanne wameuwawa wakati wanajeshi wa Syria wakisaidiwa na magari ya deraya walipoushambulia mji wa Deraa kwa mabomu alfajiri ya leo. Kwa mujibu wa wakaazi na wanaharakati wa upinzani, milio ya milipuko na bunduki za rashasha imesikika katika vitongoji vya al-Balad, al-Mahatta na al-Sad vya mji huo ulioko katika mpaka na Jordan, huku vikosi vya serikali vikiwashambulia waasi.
Marekani imepuuzilia mbali ahadi ya kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchini Syria, ikiitaja kuwa kichekesho. Msemaji wa ikulu ya Marekani, Jay Carney, amesema ahadi hiyo inakejeli mapinduzi nchini Syria. Msemaji huyo pia amesema ahadi za mageuzi zimekuwa zikifuatiwa na ongezeko la machafuko na hazijawahi kutimizwa na utawala wa Syria, tangu kuanza kwa maandamano ya amani nchini humo.
Hapo jana rais wa Syria, Bashar al Assad, kwa haraka aliamuru kura ya maoni ifanyike wiki mbili zijazo kuhusu pendekezo la katiba mpya itakayoviruhusu vyama vya kisiasa mbali na chama cha Baath, kushiriki katika chaguzi. Upinzani wa Syria umeipinga vikali hatua hiyo na kuwataka Wasyria waikatae na kuigomea kura hiyo ya maoni.
Akizungumza jana akiwa ziarani nchini Brazil, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alisema mapendekezo yote ya rais Assad yatachunguzwa kwa makini, lakini mbinu za kijanja anazozitumia hazitakubalika.
"Cha muhimu kwetu ni njia iwekwe wazi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kidemokrasia na machafuko yakomeshwe. Machafuko yanafanywa na utawala wa Assad. Anabeba dhamana na lazima ang'atuke."
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuijadili Syria
Wakati huo huo, baraza kuu la Umoja wa Mataifa linakutana leo kujadili pendekezo la azimio lililoandaliwa chini ya uongozi wa Saudi Arabia, linalolaani machafuko yanayoendelea Syria na linalotaka mageuzi ya kisiasa kuelekea mfumo wa demokrasia.
Azimio hilo linajumuisha lugha iliyotumika katika azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lililopingwa na Urusi na China kutumia kura zao za turufu mnamo tarehe 14 mwezi huu. Hakuna mamlaka ya kura ya turufu katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo nchi 193 wanachama zina kura sawa.
Iwapo baraza kuu litaridhia azimio hilo, itakuwa mara ya pili tangu Desemba mwaka jana kwa baraza hilo kulaani ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria.
Kwa upande mwingine, Uswisi imesema itaufunga ubalozi wake mjini Damascus na imewataka raia wake waondoke Syria haraka iwezekanavyo. Uswisi ilimuondoa balozi wake kutoka Syria baada ya kuanza kwa ukandamizaji, lakini iliuacha wazi ubalozi wake ili kuwasaidia raia wake kati ya 150 na 180 wanaoishi nchini humo, wengi wao wakiwa na uraia wa nchi mbili.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE
Mhariri: Daniel Gakuba