1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Syria vyazidi kusonga mbele Palmyra

29 Machi 2016

Vikosi vya serikali ya Syria vikisaidiwa kwa mashambulizi ya ndege za kivita za Urusi, vimeendelea kupambana na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu-IS kwenye mji wa Palmyra.

Syrien Palmyra Syrische Armee erobert Zitadelle
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Sharifulin

Vikosi hivyo vinazidi kusonga mbele kuelekea kwenye jimbo la Deir Ezzor, ambalo ni ngome ya IS, siku moja baada ya kuchukua tena udhibiti wa mji wa kale, Palmyra, ambao majengo yake yalibomolewa na IS. Rais wa Syria, Bashar al-Assad amesema kukombolewa mji wa Palmyra kutoka kwa wapiganaji wa IS ni ushindi mkubwa katika mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi duniani.

Iran, mshirika mwingine muhimu wa Rais Assad, imepongeza hatua ya kukombolewa mji wa Palmyra na imeahidi kuendelea kuisaidia Syria kifedha na kijeshi. Jeshi la Syria limesema mji huo uliokombolewa utatumika kama jukwaa la kuendesha operesheni dhidi ya ngome imara za IS mjini Raqqa na Deir al-Zor.

Shirika linalofatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake Uingereza, limesema mapambano yameendelea kaskazini mashariki mwa Palmyra kati ya IS na vikosi washirika kwa serikali, vikisaidiwa na jeshi la wanaanga la Syria na Urusi. Kwa mujibu wa shirika hilo, mashambulizi ya anga pia yaliilenga barabara kutoka Palmyra

Moja ya majengo ya maonyesho ya kale ya PalmyraPicha: Getty Images/AFP/M. Al Mounes

inayoelekea mashariki mwa Deir al-Zor na mapigano yanaendelea kwenye mji wa Qaryatain unaoshikiliwa na IS. Serikali ya Syria imekuwa ikijaribu kuukomboa mji wa Qaryatain tangu ulipotekwa na IS mwezi Agosti mwaka uliopita.

Marekani yahofia utawala wa Assad

Marekani imepongeza hatua iliyofikiwa na vikosi vya Syria kwa tahadhari, huku msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, John Kirby akisema nchi yake haifikirii kwamba ushindi huo dhidi ya IS utakuwa ufumbuzi wa muda mrefu. Marekani pia inahofia rekodi ya utawala wa kikatili wa Rais Assad.

''Tunadhani ni jambo zuri kwamba IS hawana udhibiti tena. Lakini bila shaka tunatilia maanani kwamba njia bora kwa Syria na watu wa Syria siyo kuongeza uwezo wa Bashar al-Assad kuendeleza utawala wa kikatili kwa watu wa Syria,'' alisema Kirby.

Kukombolewa kwa mji wa Palmyra ni pigo kubwa kwa kundi hilo la jihadi, tangu lilipojitangazia uongozi wa ukhalifa mwaka 2014 katika maeneo mengi ya Syria na Iraq na ni mapinduzi makubwa kwa Syria na Urusi.

Rais Bashar al-AssadPicha: picture alliance/dpa/SANA

IS imeuharibu mji huo kwa kuyabomoa makaburi na mahekalu kadhaa, wakati wa udhibiti wake wa miezi 10. Mji huo uko katika orodha ya turathi za dunia za shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni-UNESCO na unajulikana kama 'Lulu ya Jangwani'.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry ameapa kuongeza shinikizo zaidi dhidi ya IS baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu mjini Washington.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,RTR
Mhariri: Hamidou Oumilkheir

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW