1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Ukraine vyang'ang'ana mjini Severodonetsk

Daniel Gakuba
10 Juni 2022

Ukraine imesema vikosi vyake vinakabiliwa na mashambulizi makali ya Urusi, wakati vikijitahidi kushikilia ngome zao katika maeneo muhimu ya mji wa Severodonetsk.

Ukraine-Krieg | Zerstörung in Bachmut
Picha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Tangazo la kamandi ya jeshi la Ukraine limesema kuwa vikosi vya mizinga vya Urusi vimefanya operesheni za mashambulizi dhidi ya ngome za Ukraine katika mji wa Severodonetsk hata hivyo bila mafanikio makubwa, na kwamba vikosi vya Ukraine vilikuwa vikiwazuia wanajeshi wa msaada wa Urusi walioletwa kutoka vijiji jirani na mji huo wa ukanda wa Donbas.

Soma zaidi: Rais Zelensky asema ushindi utakuwa wao dhidi ya uvamizi 

Ikiwa Urusi itaukamata mji huo itaweza kuudhibiti ukanda wa Donbas, na pia mto muhimu wa Donets. Ukanda huo unavyo viwanda vingi, na kuumiliki kutaisaidia Urusi kuweka kiunganishi cha nchi kavu na rais ya Crimea iliyoinyakuwa kutoka Ukraine mwaka 2014.

Kamandi ya jeshi la Ukraine imearifu pia kuwa Urusi vile vile ilikuwa ikikusanya wanajeshi katika uelekeo wa mji mwingine muhimu wa Slovyansk, ikijiandaa kuushambulia, na kuongeza kuwa katika muda wa saa 24 zilizopita, wanajeshi wa Ukraine wamerejesha nyuma mashambulizi saba ya Urusi katika mikoa ya Donetsk na Luhansk.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy (mwenye fulana) anasisitiza kuwa mustakabali wa Ukraine utaamuliwa na Waukraine wenyewePicha: Cover-Images/IMAGO

Hukumu ya kifo kwa wapiganaji wa kigeni

Kando na uwanja wa vita, hapo jana mahakama katika kile kinachojiita 'Jamhuri ya Watu wa Donetsk' iliyojitangazia uhuru mashariki mwa Ukraine iliwahukumu raia wawili wa Uingereza na mwingine mmoja wa Moroko adhabu ya kifo.

Wanaume hao watatu walikamatwa mwezi Aprili katika mji wa Mariupol, wakipigana upande wa Ukraine.

Soma zaidi: Ukraine yawarejesha nyuma Warusi eneo la Donbas 

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imetupilia mbali hukumu hiyo iliyoilinganisha na mchezo wa kuigiza, nayo Ukraine imesema watu hao waliokuwa wakaazi halali nchini Ukraine, wanalindwa na sheria ya kimataifa kuhusu wafungwa wa kivita.

Huku hayo yakiendelea, Ukriane imeelezea hofu kuwa kadri uvamizi wa Urusi dhidi yake utakavyochukua muda mrefu, ndivyo washirika wake wa magharibi watakavyochoka kuiunga mkono katika mapambano yake dhidi ya uvamizi huo.

Mji wa Severodonetsk unakabiliwa na mashambulizi makali tangu mwishoni mwa mwezi MeiPicha: Aris Messinis/AFP

Ukraine haiambiwi chochote kuhusu kuridhia masharti ya Urusi

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekwishatupilia mbali mapendekezo ya baadhi ya nchi za magharibi juu ya yale inayoweza kuridhia ili kupata amani na Urusi, zikiwemo Ufaransa na Italia.

Hata ushauri wa waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, Henry Kissinger kwamba Ukraine ikubali kuachia baadhi ya maeneo yake kwa Urusi kwa ajili ya amani umetupiliwa mbali na Ukraine.

Soma zaidi: Ukraine lazima iamue mustakabali wake yenyewe: Duda

Zelenskiy amesema Ukraine itaamua yenyewe masharti yake katika mazungumzo na Urusi.

Wachambuzi wa masuala ya vita wanaamini Urusi itacheza mchezo wa kurefusha vita ili nchi za magharibi ziishiwe na subira, na kulazimika kuishinikiza Ukraine kukubali masharti magumu ya Urusi.

ape, rtre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW