1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Ukraine vyaondoka Severodonetsk

24 Juni 2022

Vikosi vya Ukraine vitaanza kuondoka kwenye mji wa Severodonetsk baada ya wiki kadhaa za mashambulizi makali sana ya Urusi kwenye mkoa wa mashariki wa Donbas, ishara kwamba sasa wanapoteza mji mwingine muhimu kimkakati.

Ukraine-Krieg - Kiew
Picha: Daniel Ceng Shou-Yi/ZUMA Wire/IMAGO

Baada ya mapambano ya wiki kadhaa mitaani, vikosi vya Ukraine sasa vimedhihirika kuishiwa na nguvu na silaha mbele ya vile vya Urusi. 

Kwa mujibu wa gavana wa jimbo la Luhansk, Sergiy Haiday, hakuna haja ya wanajeshi kuendelea kupigania sehemu ya mji iliyobakia ambayo kwa ujumla imegeuzwa kuwa vifusi vitupu. 

Mji wa Severodonestk ni muhimu na wa kimkakati kwa yeyote ambaye anataka kuwa na udhibiti kamili wa mkoa wa Donbas. 

Kwa Urusi kuutwaa mji huo na mwenzake wa Lysychansk, sasa kunaipa udhibiti wa jimbo zima la Luhansk, mmoja kati ya majimbo mawili yanayounda mkoa mkubwa wa kiviwanda wa Ukraine, Donbas. 

Baada ya hapo, huenda sasa Urusi ikawania kukamilisha uchukuwaji wa jimbo la Donetsk, ambalo wengi wanasema ndilo lengo kuu la uvamizi wake ulioanza mwezi Februari nchini Ukraine.

Umoja wa Ulaya waridhia uwanachama wa Ukraine

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel (kulia) akizungumza mjini Brussels baada ya kikao cha kuiridhia Ukraine kuwa mgombea uwanachama wa Umoja huo siku ya Alkhamis (Juni 23).Picha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

Hayo yakijiri, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuzipa Ukraine na jirani yake Moldovahadhi ya kugombea uwanachama wa Umoja huo, ikiwa ishara ya uungaji mkono wake dhidi ya vita vya Urusi. 

Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Charles Michel, amesema kupitia ukurasa wa Twitte na hapa namnukuu: "Hili ni tukio la kihistoria. Leo ni siku muhimu inayoashiria hatua muhimu kwenye njia yenu kuelekea Umoja wa Ulaya." Mwisho wa kunukuu.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa hatua hiyo, akisema mustakabali wa nchi yake umo ndani ya Umoja wa Ulaya.

"Imetambuliwa rasmi kwamba Ukraine si daraja, si mto baina ya Magharibi na Urusi, si eneo la kuzitenganisha Ulaya na Asia, sio eneo la kusaka ushawishi, si eneo lisilo upande, si mamlaka ya mpito. Wala si mpaka baina ya mazimwi na majini. Ukraine ni mshirika ajaye mwenye haki sawa na nchi 27 za Umoja wa Ulaya. Ukraine ni mgombea wa kujiunga na Umoja wa Ulaya." Alisema rais huyo.

Hata hivyo, kupata hadhi ya kuwa mgombea ni jambo moja na kuwa mwanachama kamili ni kitu chengine, kwani katikati yake pana mchakato unaoweza kuchukuwa miaka mingi kabla ya kukamilika, kama ilivyo mifano ya Uturuki na mataifa mengine yenye hadhi kama hiyo.

Kwa upande mwengine, Marekani inatuma msaada mpya wa kijeshi wenye dhamani ya dola milioni 450 kwa Ukraine, ikiwemo mifumo minne ya makombora dhidi ya vikosi vya Urusi.