Vikosi vya Ukraine vyauzuwia msafara wa Urusi kuvuka mto
13 Mei 2022Urusi imekumbana na vizuwizi kwenye medani ya vita huku Ukraine ikiwafurusha wanajeshi wake kutoka maeneo yalio karibu na mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv, katika usongaji mbele wa kasi zaidi tangu kuvilazimisha vikosi vya Kremlin kuondoka Kyiv na kaskazini mashariki zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
Soma pia: Idadi ya waliokimbia Ukraine yavuka watu milioni 6
Waandishi wa habari wa Reuters wamethibitisha kuwa Ukraine sasa inadhibiti eneo linaloenea hadi ukingo wa Mto Siverskiy Donets, umbali wa karibu kilomita 40 mashariki mwa Kharkiv.
Ukanda wa video uliotolewa na kamandi ya kikosi cha anga cha Ukraine ulionekana kuonyesha magari kadhaa ya kijeshi yaliyoteketezwa na sehemu za daraja zilizozama kwa kiasi katika mto huo.
Picha hizo zilionyesha magari mengi zaidi yaliyoharibika au kutelekezwa, vikiwemo vifaru, yakiwa msituni na kwenye njia inayoelekea mtoni.
Soma pia: Umoja wa Mataifa kuamua juu ya uchunguzi Ukraine
Ikitoa taarifa za kijasusi za kila siku ya Ijumaa, wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema picha hizo zinaonyesha kuwa Urusi imepoteza alau kundi moja la kikosi cha mbinu za kijeshi na vifaa vya daraja la pantoni viliharibiwa wakati wa kuvuka mto Siverskyi Donets magharibi mwa Severodonetsk.
Wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema Urusi inawekeza juhudi kubwa za kijeshi kusini zaidi kutoka Kharkiv, karibu Izium na Severodonetsk, na ilikuwa ikijaribu kuvunja vizuwizi kuelekea Sloviansk na Kramatorsk.
Miito ya kuokolewa wapiganaji Azovstal
Katika mji mkuu wa Kyiv, wake na jamaa za wapiganaji wa Ukraine waliojichimbia kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal katika bandari ya kusini ya Mariupol waliandamana kudai kuokolewa kwa jamaa zao.
Vikosi vya Urusi vimekuwa vikishambulia kiwanda hicho, ambacho ndiyo ngome ya mwisho ya kikosi kinachojiita watetezi wa Ukraine katika mji unaotawaliwa kabisa na Urusi baada ya kuzingirwa kwa zaidi ya miezi miwili.
Soma pia: EU na Japan kuzidisha mbinyo dhidi ya Urusi
"Nawataka watetezi wote waliopo huko warudi nyumbani ili waishi maisha ya kawaida na watoto na ndugu zao. Kwa nini wengine wanaweza kutembea mitaani na wapendwa wao na wao hawawezi? Mbona hakuna anayewasaidia?", alihoji Maria Zimareva, ambaye kaka yake ni mmoja wa wapiganaji waliojichimbia kiwandani humo.
Naibu Waziri Mkuu Iryna Vereshchuk alikiambia kituo cha televisheni cha 1+1 kwamba mazungumzo yalikuwa yakiendelea kwa ajili ya kuwaondoa wapiganaji hao, kuanzia wale waliojeruhiwa vibaya zaidi.
Mwanajeshi wa Urusi kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita Kyiv
Mjini Kyiv, mahakama inatazamiwa hii leo kuanza kusikiliza kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita tangu vita kuanza mwezi Februari.
Soma pia: Ukraine inataka kuhakikishiwa nafasi Umoja wa Ulaya
Mwanajeshi wa Urusi anatarajiwa kufikishwa mahakamani akishtakiwa kwa mauaji ya raia huko Chupakhivka, kaskazini mashariki mwa Ukraine, Februari 28.
Na huko katika kisiwa cha Nyoka ambako mapigano makali yanaendelea kuwania udhibiti wa pwani ya Bahari Nyeusi, vikosi vya Ukraine vimesema vimeharibu meli ya ugavi ya Urusi karibu na kisiwa hicho na kisha kuitia moto.
Wakati mapigano yakiendelea kote nchini, mataifa yanalenga kumuongezea shinikizo Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Soma pia: Ukraine: Zaidi ya wapiganaji 1,000 bado wamekwama Mariupol
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi la mataifa tajiri, G7, wanalenga kutoa kile Ujerumani ilichokiita "ishara yenye nguvu ya umoja" wanapokutana leo Ijumaa kujadili mzozo huo wanaohofia kuwa huenda ukasambaa hadi Moldova.
Mpango wa Finland kuomba uanachama wa NATO, uliotangazwa jana Alhamisi, na matarajio kwamba Sweden itafuata mkondo huo, italeta upanuzi wa muungano huo wa kijeshi wa Magharibi ambao Putin alilenga kuuzuia.
Ikulu ya Kremlin imeonya kuwa hatua ya mataifa hayo mawili kujiunga na NATO itajibiwa vikali.
Chanzo: Mashirika