1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Urusi vinazidi kusonga mbele mjini Mariupol

Sylvia Mwehozi
20 Machi 2022

Vikosi vya Urusi vimezidi kusonga mbele zaidi katika mji wa bandari uliozingirwa wa Mariupol ambako mapigano makali ya Jumamosi yalifunga kiwanda kikubwa cha chuma na mamlaka za mji kuomba msaada zaidi kutoka magharibi.

BG Ukraine Situation im Kriegsgebiet
Picha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Kuanguka kwa Mariupol, kutaashiria ushindi mkubwa kwa wapiganaji wa Urusi ambao kwa kiasi kikubwa wamekwama nje ya miji mikubwa, wiki tatu baada ya uvamizi mkubwa barani Ulaya tangu vita ya pili ya dunia.

Uhamishaji wa raia kutoka mikoa iliyozingirwa umeendelea siku ya Jumamosi kupitia njia 10 salama za kiutu. Afisa wa polisi wa Mariupol Michail Vershnin amedai kuwa mji huo umeharibiwa na kuteketezwa. "Watoto na wazee wanakufa", amesema afisa huyo wakati akizungumza na viongozi wa Ulaya kwa njia ya video. Nalo baraza la mji wa Mariupol limesema kwamba wanajeshi wa Urusi wanawalazimisha maelfu ya wakaazi wa mji huo kuelekea Urusi.

Uharibifu wa jengo mjini MariupolPicha: REUTERS

Taarifa kutoka mji wa Kharkiv zinasema kwamba takribani raia 260 wameuawa tangu kuanza kwa uvamizi. Miongoni mwa hao wapo watoto 14. Mji huo ulioko Kaskazini mashariki mwa Ukraine umezingirwa pia na vikosi vya Urusi. Umeendelea kushambuliwa kwa mizinga mikubwa huku majengo ya makaazi ya raia yakishika moto siku ya Jumamosi.

Zelensky na wito wa mazungumzo

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwa mara nyingine siku ya Jumamosi alitoa rai ya mazungumzo ya kina na Moscow na pia akaitaka Uswisi kufanya kila linalowezekana kuwaadhibu vigogo wa Urusi ambao amedai wanasaidia kufadhili vita inayoendelea kupitia pesa zao.

Zelenskiy, ambaye mara kwa mara amekuwa akitoa wito wa kuomba msaada kwa mataifa ya kigeni, aliwaeleza waandamanaji mjini Bern waliokuwa wakipinga vita kwamba benki za Uswisi zilikuwa na "fedha za watu ambao walianzisha vita hivi" na akaunti zao zinapaswa kufungwa.

Miji ya Ukraine "inaharibiwa kwa amri ya watu wanaoishi Ulaya, katika miji mizuri ya Uswisi, wanaofurahia mali katika miji yenu. Ingekuwa vizuri kuwaondolea hadhi hii," alisema Zelensky.

Putin na Scholz wazungumza tena kuhusu Ukraine

01:16

This browser does not support the video element.

Taarifa za kijasusi zilizotolewa na Uingereza zimeonya kwamba Urusi ambayo imekatishwa tamaa na kushindwa kufikia malengo yake tangu ilipoanzisha uvamizi Februari 24, sasa inajaribu kutumia mkakati wa udhoofishaji kwa kuwashambulia raia na hivyo kuzidisha mzozo wa kiutu.Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine

Uswizi isiyoegemea upande wowote, ambayo si mwanachama wa Umoja wa Ulaya imepitisha kikamilifu vikwazo vya muungano huo dhidi ya watu binafsi wa Urusi na taasisi, ikiwa ni pamoja na kufungia mali katika benki za Uswisi.

Siku ya Jumamosi, Urusi ilisema makombora yake ya Hypersonic yameharibu bohari kubwa ya chini ya ardhi ya makombora na ndege katika mkoa wa magharibi wa Ivano-Frankivsk.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW