1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Urusi vyadai kutwaa udhibiti ngome ya Ukraine

20 Mei 2024

Urusi imetangaza kuchukua udhibiti kamili katika eneo la Ukraine la Bilohorivka huku mamlaka za miji ya Kherson na Zaporizhia zikisema watu wawili wamekufa kufuatia shambulizi la Urusi leo

 Kharkiv Ukraine
Wakaazi katika Mkoa wa kharkiv wakiwa wanayahama makazi yao kufuatia mashambulizi ya Urusi katika eneo hiloPicha: ZUMAPRESS.com/picture alliance

     
Watu wawili wamekufa kufuatia shambulizi la Urusi katika miji ya Kherson na Zaporizhia iliyopo kusini mwa Ukraine. Urusi imeendeleza mashambulizi yake huku ikitangaza kuchukua udhibiti kamili katika eneo la Ukraine la Bilohorivka ingawa Ukraine inadai kwamba wanajeshi wake wapo katika hatua nzuri ya mapamabano katika maeneo hayo ya mpakani.

Soma zaidi.Mashambulizi ya Urusi yawaua watu 11 mjini Kharkiv 

Gavana wa mji wa Kherson Oleksandr Prokudin akieleza tathmini ya mashambulizi ya Urusi katika eneo hilo ametangaza kutokea kwa vifo hivyo katika mji huo wa kusini mwa Ukraine.Vikosi vya Ukraine viliukomboa mji huo wa mpakani kutoka kwa vikosi vya Urusi mwishoni mwa mwaka 2022 lakini sehemu kubwa ya eneo lake imeendelea kushuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa vikosi vya Urusi.

Picha inayoonyesha uharibifu uliofanywa na shambulizi la Urusi katika mkoa wa Kharkiv nchini UkrainePicha: Anadolu/picture alliance

Kwa upande wake jeshi la Urusi limetangaza hii leo kuchukua udhibiti kamili katikia eneo la Bilohorivka katika mkoa wa Luhansk hatua ambayo jeshi la Urusi imeitaja kuwa ni muhimu zaidi katika mapambano yao dhidi ya vikosi vya Ukraine.

Soma zaidi. Ukraine yashambulia Crimea kwa droni

Wizara ya Ulinzi ya Urusi nayo imesema katika taarifa yake kuwa vikosi ya Urusi leo pia vilihusika katika mapigano makali katika mji wa Kharkiv na kwamba operesheni yao ya maeneo ya mipakani bado inaendelea.

Zelensky: Tunazidi kusonga mbele kwenye uwanja wa vita

Mamlaka katika mji wa Kharkiv zimesema kwa sasa vikosi vya Ukraine vinadhibiti kwa asilimia 60 maeneo yaliyopo mpakani katika upande wa mashariki ambalo linakabiliwa na mashambulizi mfululizo ya Urusi.

Kauli hiyo ya mamlaka ya Ukraine imeungwa mkono pia na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye amesema kuwa jeshi lake limepata nguvu zaidi katika mikoa ya Kharkiv na Donetsk.

Rais wa Ukraine Voldymyr Zelensky akiwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony BlinkenPicha: Brendan Smialowski/REUTERS

"Leo, kama ilivyo kila siku, lengo letu la msingi ni katika maeneo yote ya upinzani na kwenye safu nzima ya ulinzi. Kulikuwa na ripoti kutoka kwa kamanda mkuu. Jenerali Syrskyi yuko mstari wa mbele, moja kwa moja na vikosi vyetu vya mapigano. Na matokeo yake ni kuwa tumepata nafasi zenye nguvu zaidi katika eneo la Kharkiv Brigade ya 57, Brigedi ya 82 ya Mashambulizi ya Anga: Asanteni , wapiganaji''. Amesema Zelensky.

Soma zaidi. Zelensky: Hali ya utulivu imeanza kurejea katika mkoa wa Kharkiv

Tangu mwanzoni mwa mwezi Mei vikosi vya Urusi vimefanya mashambulizi ya ardhini katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Ukraine, ambako vimeyadhibiti maeneo makubwa katika kipindi cha miezi 18. Huku kwa upande Ukraine ikadai kwamba imevirudisha nyuma vikosi vya Urusi, madai yanayopingwa na Moscow ambayo inasema kuwa inazidi kusonga mbele zaidi upande wa adui. 

Mwandishi: Suleman Mwiru 
Vyanzo: Reuters na AFP
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW