Vikosi vya Urusi vyadaiwa kuharibu eneo la viwanda la Donbas
20 Mei 2022Zelenskiy amevishtumu vikosi vya Urusi kwa kujaribu kuwauwa raia wengi wa Ukraine na kufanya uharibifu mkubwa iwezekanavyo huku akirudia madai yake kwamba Urusi inafanya mauaji ya kimbari. Zelenskiy amesema kuwa wakati vikosi vya Ukraine vinaendelea na ukombozi wa eneo la Kharkiv Mashariki mwa Kyiv, Urusi ilikuwa inajaribu kutoa shinikizo zaidi katika eneo la Donbas, lililoko Kusini Mashariki mwa Ukraine.
Katika hotuba yake Alhamisi usiku kupitia njia ya video, Zelenskiy amesema kuwa vikosi vya jeshi la Ukraine vinaendelea kusonga mbele kukomboa eneo la Kharkiv. Lakini shinikizo linazidi huko Donbas. Zelemsky ameongeza kuwa hali ni mbaya na kwamba watu 12 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika siku moja tu.
Umoja wa Ulaya wapendekeza mkopo wa Euro bilioni 9 kwa Ukraine
Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya siku ya Jumatano ulipendekeza mkopo wa euro bilioni 9 kwa Ukraine kulisaidia taifa hilo kujiendeleza wakati linapojitahidi kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Siku ya Alhamisi, von der Leyen ameliambia shirika la habari la ZDF kwamba mawakili wao wanafanya kazi kwa bidii kutafuta njia inayowezekana ya kutumia mali hiyo ya mabwenyenye wa Urusi iliyozuiwa kwa ujenzi upya wa Ukraine huku akiongeza kuwa Urusi pia inapaswa kutoa mchango wake. Von der Leyen ameongeza kuwa anapendelea kuunganishwa kwa ujenzi mpya wa muda mrefu wa Ukraine na mageuzi yanayohitajika kwa taifa hilo kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Huku hayo yakijiri, wanasheria wakuu wa mataifa wanachama wa muungano wa kijasusi unaojulikana kama "Macho Matano" Alhamisi wameunga mkono vikali juhudi za Ukraine za kushtaki uhalifu wa kivita unaotokana na uvamizi wa Urusi. Wanasheria hao wakuu wa Uingereza, Marekani, Australia, Canada na New Zealand wamesema wanamuunga mkono kikamilifu mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine Iryna Venediktova katika kuhakikisha uwajibikaji kwa uhalifu wa kivita uliotendwa tangu Urusi iliposhambulia nchi hiyo mnamo Februari 24.
Katika taarifa, wanasheria hao wakuu wamesema kuwa wanaunga mkono utafutaji wa haki wa Ukraine kupitia uchunguzi mwingine wa kimataifa unaojumuisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na taasisi nyingine. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa wanailaani Urusi kwa vitendo vyake na kuitaka ikomeshe ukiukaji wote wa sheria za kimataifa, kukomesha uvamizi wake haramu na kushirikiana katika juhudi za kufikia uwajibikaji. Mamlaka ya Ukraine imesema imefungua maelfu ya kesi za madai ya uhalifu uliofanywa na vikosi vya Urusi.