1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya usalama Myanmar vyaendeleza matumizi ya nguvu

15 Machi 2021

Watu wawili wameuawa Jumatatu Myanmar, baada ya vikosi vya usalama nchini humo kuendelea kutumia nguvu kuyatawanya maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi kwenye mji wa Yangon.

Weltspiegel 15.03.2021 | Myanmar nach Militärputsch | Yangon, Verletzter
Picha: REUTERS

Watu walioshuhudia wamesema wafuasi wa kiongozi wa kiraia aliyepinduliwa, Aung San Suu Kyi wameandamana tena Jumatatu kwenye miji kadhaa ya Myanmar ikiwemo Mandalay na kwenye mji wa kati wa Myingyan, ambako polisi walifyatua risasi kuwatawanya waandamanaji. Mtu mmoja amesema polisi walimuua kwa risasi msichana mmoja kwenye kichwa na mvulana mmoja alipigwa risasi kwenye uso.

Mauaji ya leo yanafanyika mbali na yale yaliyotokea siku ya Jumapili ambayo yanaelezwa kuwa mabaya zaidi tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi Februari Mosi, ambapo watu 37 waliuawa  kwenye kitongoji cha Hlaingthaya, baada ya kutokea ghasia kwenye viwanda vinavyomilikiwa na raia wa kigeni na hasa wa kutoka China, ambako polisi na wanajeshi wa eneo hilo walikabiliana na waandamanaji waliokuwa wamejihami na fimbo na visu.

China yalaani mauaji

Ghasia hizo zimesababisha China kulaani kile kinachoendelea, ingawa wengi wanaona kuwa nchi hiyo imekuwa ikiyaunga mkono mapinduzi hayo. Ubalozi wa China umewatolea wito majenerali wa kijeshi wanaotawala Myanmar kuacha kutumia nguvu na kuhakikisha usalama kwa watu wake pamoja na mali zao. Gazeti la China la Global Times limeripoti kuwa viwanda 32 vya Wachina viliharibiwa katika ghasia ambazo zimesababisha hasara ya dola milioni 37 na wafanyakazi wawili wa Kichina kujeruhiwa.

Wanajeshi wakipiga doria kwenye mji wa YangonPicha: REUTERS

Japan kwa upande wake imesema inaifatilia kwa karibu hali inayoendelea Myanmar na inafikiria jinsi ya kulishughulikia suala hilo katika muktadha wa ushirikiano wa kiuchumi.

Huku hayo yakiarifiwa, Myanmar imetangaza sheria ya kijeshi katika maeneo kadhaa yenye idadi kubwa ya watu mjini Yangon. Hatua hiyo katika vitongoji vya Hlaing Tharyar, Shwe Pyi Thar, Okkalapa Kaskazini, Dagon Kaskazini, Dagon Kusini na Dagon Seikkan, imechukuliwa kutokana na umwagikaji mkubwa wa damu uliofanyika Jumapili.

Umoja wa Mataifa wataka ushirikiano wa jumuia ya kimataifa

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Myanmar, Christine Schraner Burgener amelaani vikali mauaji hayo na ameitaka jumuiya ya kimataifa, wakiwemo wadau wa kikanda, kushirikiana pamoja na kuoneshe mshikamano na watu wa Myanmar na ari yao ya kudai demokrasia.

Wakati huo huo, mahakama moja nchini Myanmar imeshindwa kufanya kikao cha kesi inayomkabili Suu Kyi leo kwa sababu ya matatizo ya mtandao wa intaneti. Kiongozi wa timu ya mawakili, wa Suu Kyi, Khin Maung Zaw amesema kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 24 mwezi huu.

''Kesi hii haikuweza kusikilizwa leo kwa sababu ya matatizo ya mtandao wa intaneti nchini kote. Kikao cha kusikiliza kesi ya Bibi Suu Kyi kinafanyika tu kwa njia ya video, hivyo leo kikao hakiwezi kufanyika kwa sababu hakuna intaneti,'' alifafanua Zaw. Suu Kyi anakabiliwa na takriban mashtaka manne.

(DPA, AP, AFP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW