Vikosi vya Uturuki vyashambulia waasi wa Kikurd nchini Irak
23 Februari 2008ANKARA:
Maafisa wa kijeshi nchini Uturuki wanasema,wanamgambo 24 wa Kikurdi na wanajeshi wake 5 wameuawa katika mapigano kaskazini mwa Irak.Hapo awali,jeshi Uturuki lilithibitisha kuwa zaidi ya wanajeshi wake 10,000 wameingia ndani ya ardhi ya Irak kuwasaka waasi wa Kikurd wa chama cha PKK wanaotumia eneo hilo la milimani kuishambulia Uturuki.
Wakuu wa serikali ya Irak wamelalamika kuhusu uvamizi huo,kaskazini mwa nchi yao,lakini wanasema ni wanajeshi mia kdhaa tu waliovuka mpaka.Wengine walizuiliwa na vikosi vya Wakurd wa Irak wenye utawala wa ndani katika eneo hilo la kaskazini ambalo hasa hukaliwa na Wairaki wenye asili ya Kikurdi.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameihimiza Uturuki kuheshimu mpaka wa Irak.Vile vile ametoa mwito kwa chama cha PKK kusita kuishambulia Uturuki.