1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo dhidi ya Zimbabwe vyamuumiza nani?

22 Novemba 2010

Neno vikwazo lilikuwa miongoni mwa maneno yaliyotajwa na balozi mpya wa Umoja wa Ulaya nchini Zimbabwe, Aldo Dell Ariccia, mara tu alipowasili nchini humo na kukutana na viongozi wa serikali miezi michache iliyopita

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Wanasiasa nchini humo wamejaribu kuwashawishi Wazimbabwe na watu wa nje kwamba vikwazo vilivyowekwa kwa raia 98 wa nchi hiyo na baadhi ya makampuni, vimechangia kwa kiasi kikubwa kuanguka kwa uchumi wa Zimbabwe na kushuka kwa maisha.

Mnamo mwaka 2002, Umoja ya Ulaya ilimuwekea vikwazo Rais Robert Mugabe na wanachama wenzake wa chama cha ZANU-PF pamoja na jeshi la nchi hiyo, polisi, mahakimu na baadhi ya watu pamoja na makumpuni yaliyokuwa na uhusiano na serikali pamoja na chama tawala. Vikwazo hivyo vinahusika moja kwa moja katika kufifisha haki za binadamu na hali ya kisiasa nchini humo.

Masharti katika vikwazo hivyo vilivyowekewa Zimbabwe ni pamoja na kuzuiliwa kuingia katika nchi za Umoja ya Ulaya, kuzuiliwa kwa mali zao, matumizi ya silaha na vifaa vyovyote vinavyoweza kutumika kwa ukandamizaji.

Wagonjwa wa kipindupindu nchini ZimbabwePicha: AP

Dell Ariccia amefafanua vipengele vilivyowadhibiti viongozi wa chama cha ZANU-PF na wote waliowekewa vikwazo havijawekwa kuwaumiza wananchi wa kawaida wa nchi hii ila vinawalenga wale waliokaribu na chama kilichopo madarakani.

"Kwa kuthibitisha hili Umoja wa Ulaya utabaki Zimbabwe na kuifanya kuwa mshirika wake wa pili kibiashara baada ya Afrika ya Kusini."

Kwa msisitizo, Dell Ariccia alisema kuwa Umoja wa Ulaya unatoa kiasi cha dola milioni 18 kusaidia kuinua sekta ya sukari na unajihusisha na shughuli mbalimbali za kibinadamu nchini humo.

Kwa upande wake, mwanahistoria wa uchumi Dk. Tafataona Mahoso, ametofautiana na balozi huyo na kusema vikwazo hivyo ni vita vya kiuchumi kwa wananchi wa Zimbabwe, na kuitaja hali hiyo kama iliyorudisha nyuma maisha ya wananchi sawa na kipindi cha miaka ya 1953.

Mahoso ametolea mfano kwa mamilioni ya Wazimbabwe ambao wamekimbilia nchi jirani na nchi za Magharibi, ambako wanalazimika kufanya kazi ambazo si za maana kama vile kazi za nyumbani. Anasema, lau kama wangekuwa nchini mwao, Wazimbabwe hawa wasingezifanya kazi hizo na hiyo ndio athari ya vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimeshuhudia watu wakipoteza viinua mgongo vyao na utu wao.

Kwa kuangalia jinsi gani uchumi wa nchi hiyo ulivyoathirika kutokana na vikwazo, Mahoso ameeleza kuwa makampuni nchini Zimbabwe hayawezi kuingiza vifaa kutoka nje ya nchi kwa sababu yamezuiliwa. Serikali ya Zimbabwe inajaribu kutoa huduma muhimu, kwani inalazimika kufuata uchumi unaotegemea fedha taslimu.

Uchumi wa vikwazo unazalisha watu wenye vikwazo. Uchumi ni kama mto, yeyote atakaeweka vikwazo vya kiuchumi katika nchi, ni sawasawa na kuweka sumu kwenye mto ambao yeyote anayetumia maji ya mto huo, basi bila shaka atadhurika.

Inaaminika kwamba matokea ya uchaguzi wa uraisi ya mwaka 2008 yalikuwa na hila ya kuzuia ushindi wa chama cha Movement for Democratic Change kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai.

Mwandishi: Fatuma Matulanga/AFP

Mhariri: Saumu Mwasimba

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW