Vikwazo vipya dhidi ya Iran vyazua wasiwasi
13 Mei 2018Baada ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vipya, na wakati huo huo rais Donald Trump kutoa vitisho kwamba kampuni yoyote ya nje itakayofanya biashara nchini Iran itadhibiwa, hatua hiyo imesababisha wasiwasi mkubwa kwa makampuni ya Ulaya.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema hofu yao ni ya msingi kabisa ambapo ameonya kwamba itakuwa vigumu kuwalinda wafanyabiashara wa Ujerumani watakaoendelea kufanya biashara nchini Iran.
Maas ameliambia gazeti la Ujerumani la ‘Bild am Sontag' kwamba haoni njia nyepesi ya kupata suluhuhisho kwa ajili ya kuwalinda wafanyabiashara hao ili kuepukana na athari zitakazotokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Siku ya Jumanne, rais wa Marekani Donald Trump aliamua kuiondoa nchi yake kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran uliofikiwa mwaka 2015 na kutia saini amri ya kuiwekea vikwazo vipya Iran.
Licha ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kuapa kwamba zitaendelea kuuenzi mkataba huo, wafanyabiashara wa barani Ulaya wapo kwenye njia panda kwa kuwa makampuni ya nje yatakabiliwa na adhabu baada ya vikwazo hivyo vya Marekani kuanza kutekelezwa. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema washirika wa Ulaya wanatafuta njia za kuhakikisha Iran itaendelea kufuata makubaliano ya mpango wa nyuklia yaliyofikiwa.
Bwana Maas pia alielezea msimamo wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuwa mpango huo unapaswa kujadiliwa kwa upana zaidi ili kushughulikia jukumu na matatizo ya Iran katika mashariki ya Kati.
Waziri Heiko Maas amesema baada ya yote, Iran iko tayari kufanya mazungumzo na ni dhahiri kuwa ni lazima kuwepo na motisha katika uchumi wa nchi hiyo lakini hata hivyo haitakuwa rahisi hayo yote kufanyika hasa baada ya uamuzi wa Marekani. Kwa upande wake balozi wa Marekani nchini Ujerumani Richard Grenell amesema hakutakuwepo vita vya kibiashara kati ya Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf Scholz alizungumza na mwenzake wa Marekani Steve Mnuchin ili kuweka uwezekano wa kupata msamaha kwa makampuni ya Ujerumani kutokana na adhabu zitakazotolewa na Marekani iwapo makampuni hayo yataendelea kufanya biashara na Iran hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani la Handelsblatt katika taarifa yake iliyochapishwa siku ya Ijumaa.
Makubaliano ya mwaka 2015 kati ya nchi sita zenye nguvu na Iran yalimaanisha kuwa vikwazo vya kimataifa vingeweza kuondolewa na badala yake Iran ikubali kupunguza viwango katika mpango wake wa nyuklia. Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, atakutana na kufanya mazungumzo na wenzake wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza huko mjini Brussels siku ya Jumanne ijayo.
Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/2xcE3
Mhariri: Lilian Mtono