1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vipya dhidi ya Urusi ni vikali kiasi gani?

25 Februari 2022

Wakati Urusi ikiivamia Ukraine, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeandaa vikwazo vipya vinavyolenga kuuadhibu utawala wa Rais Vladmir Putin. Wanalenga matumizi ya dola ya Urusi kupitia benki zake kubwa na kampuni muhimu. 

Ukraine-Konflikt | PK des US-Präsidenten Biden
Picha: Brendan Smialowski/AFP

Mara tu Urusi ilipoanzisha mashambulizi yake makubwa dhidi ya Ukraine Alhamisi asubuhi, uvumi uliongezeka kuhusu Marekani, Umoja wa Ulaya na Jumuia ya Kujihami ya NATO wangejibu kwa njia ya vikwazo. Vikwazo kadhaa tayari vilikuwa vimetangazwa siku ya Jumatano, baada ya Rais Putin kuyaamuru majeshi yake kuingia kwenye majimbo ya Donetsk na Luhansk ambayo yanadhibitiwa na watu wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Hatua hizo zilikosolewa na wachambuzi kadhaa kwamba sio kali na hazina athari yoyote kwa Urusi, na kusababisha mapendekezo kwamba vikwazo vikali zaidi vitawekwa iwapo Urusi itaivamia kabisa Ukraine. Wakati Putin alipoivamia kijeshi Ukraine Alhamisi, Marekani na washirika wake walitangaza vikwazo vipya kadhaa vinavyoelezwa kuwa vikali.

Kuzilenga benki kubwa zaidi

Akizungumza mubashara kwa njia ya televisheni, jana Rais wa Marekani, Joe Biden alitangaza hatua kadhaa za kuchukua akisema zitakuwa na gharama kubwa kwa uchumi wa Urusi sasa na baada ya muda.

Ingawa wimbi la kwanza la vikwazo vya Marekani lilizikumba taasisi ndogo za fedha, awamu hii imezigusa benki kubwa mbili za Urusi ambazo ni Sberbank na VTB Bank, zote zinamilikiwa na serikali.

Makao makuu ya Benki ya Sberbank ya Urusi iliyoko katika mtaa wa Vavilova, MoscowPicha: Alexander Shcherbak/Tass/dpa/picture alliance

Vikwazo hivyo pia vimezilenga taasisi nyingine tatu kubwa za kifedha za Urusi, Otkritie, Novikom na Sovcom, pamoja na chini ya taasisi tanzu 90 za kifedha ulimwenguni kote zinazofungamana na benki zilizowekewa vikwazo.

Kwa mujibu wa wizara ya fedha ya Marekani, kwa kuzilenga benki hizo kubwa za Urusi, vikwazo hivyo vitakuwa na athari kubwa na ya kudumu kwa uchumi na mfumo wa fedha wa Urusi.

Wakati huo huo, viongozi wa Umoja wa Ulaya walikutana jana usiku mjini Brussels na kutoa taarifa inayosema nchi wanachama 27 zimekubaliana kuweka vikwazo vinavyohusu sekta ya fedha. Umoja huo umeweka vikwazo kwenye benki mbili za binafsi zinazofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, ikiwemo Alfa-Bank.

Uingereza imechukua hatua kama hizo kwa kuzuia mali na kuziondoa benki za Urusi katika mpango wa kubadilisha pauni ya Uingereza.

Udhibiti wa mauzo ya nje na hatua zingine

Rais Biden pia ametangaza kuzuia usafirishaji wa teknolojia muhimu, huku hatua mpya za Umoja wa Ulaya zikitarajiwa kuzuia mauzo a ndege za kivita na sehemu zinazohusiana na Urusi. Vikwazo zaidi vya usafirishaji vitalenga teknolojia inayohitajika ili kuimarisha matanki ya kusafishia mafuta.

Meli yenye matanki ya gesi katika mkoa wa Sakhalin, UrusiPicha: Sergei Krasnoukhov/dpa/TASS/picture alliance

Pamekuwa na uvumi mkubwa kwamba Urusi inaweza kufungiwa nje ya mfumo wa malipo ya SWIFT, ambao unaruhusu miamala ya kibenki kote ulimwenguni. Hata hivyo, inaonekana kwamba washirika wa Marekani wamesita kuitumia hatua hiyo, kutokana na upinzani kutoka kwenye nchi kadhaa za Ulaya ikiwemo Ujerumani.

Alexandra Vacroux, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Davis cha Masomo ya Kirusi na Ulaya na Asia katika Chuo Kikuu cha Havard, ameiambia DW kwamba chaguo la SWIFT litakuwa na athari kubwa sana kwa Urusi.

Anasema kupunguza uwezo wa Urusi kutumia dola kunaweza kuwa na athari sawa. Hata hivyo, ameonya kuwa hatua kali zaidi kwa Urusi pia zitaziumiza nchi za Magharibi.

Alexandra anasema Putin hatojali kuhusu athari za kiuchumi kutokana na uvamizi huu. Haitomzuia kufanya kile anachopanga kufanya. Anasema wakati huo huo, lazima umuadhibu yeye kwa namna fulani na ikiwa hautopigana naye kwa kutumia majeshi, lazima upigane naye kwa njia nyingine. Vigezo vya kiuchumi ndiyo kitu pekee walichonacho. Sio kwamba hawapaswi kutumia vikwazo vya kiuchumi, lakini hawatomzuia kuendelea kuivamia Ukraine.

(DW https://bit.ly/36JLHMh)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW