Vikwazo vya ECOWAS dhidi ya wanajeshi wa Mali
3 Aprili 2012Jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi-ECOWAS imeamua kuanzia sasa kukiweka katika hali ya tahadhari kikosi maalum cha jeshi lake-amesema rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire mwishoni mwa mkutano wa kilele mjini Dakar.Kutokana na hayo viongozi 12 waliohudhuria mkutano huo wa kilele wameitaka kamati ya wakuu wa vikosi vya wanajeshi wakutane wiki hii mjini Abidjan kutathmini namna ya kukiimarisha kikosi hicho.Tayari mwishoni mwa wiki iliyopita viongozi wa ECOWAS walisema wanajeshi 2000 wamewekwa tayari kuingilia ikilazimika nchini Mali.
Jumuia ya ECOWAS imeamua pia kupitisha "vikwazo jumla" dhidi ya utawala wa kijeshi kama walivyoahidi wakati wa mkutano wao wa Abidjan,March 29 iliyopita.Mwenyekiti wa Ecowas,rais Alassane Ouattara wa Côte d''Ivoire anasema:"Tumeamua,matokeo ya mkutano wetu wa March 29 yatatekelezwa mara moja,hadi pale CNRDRE watakaporejesha nidhamu na kuheshimu katiba.Inamaanisha hatua zote za kidiplomasia,kiuchumi,fedha na nyenginezo zitaanza kutumika mara moja na hazitabatilishwa mpaka pale katiba na taasisi zote za kidemokrasi zitakapoanza kufanya kazi kikamilifu nchini Mali."
Rais Alassane Ouattara amefurahishwa na kushiriki mkutanoni majirani wa kaskazini wa Mali, marais wa Mauritania na Algeria ambao si wanachama wa ECOWAS.
Mkuu wa utawala wa kijeshi Amadou Sanogo amesema,amesikia uamuzi uliopitishwa na kukumbusha hata hivyo kwa sasa muhimu zaidi ni kulinda umoja wa taifa.
Katika wakati ambapo vikwazo hivyo vinatangazwa,shirika la habari la ufaransa AFP linasema limepata habari za kuaminika kwamba mji mashuhuri wa kaskazini Timbuktu-umeangukia mikononi mwa wanamgambo wa kiislam wa Ansar Dine na wafuasi wa Al Qaida katika eneo la kiislam la Maghreb-AQMI.
Mkuu wa Ansar Dine,Iyad Ag Ghaly amekuja na magari 50.Wameuteka mji,wamewatimua wanamgambo wa chama cha ukombozi wa AZAWAD na kuitia moto bendera yao na badala yake kupandisha yao katika kambi ya kijeshi ya Timbuktu-amesema mpiga filamu wa AFP Moussa Haidara aliyenasa tukio hilo.Shirika la habari la Mauritania nalo limethibitisha kwamba vikosi vya AQMI vimeingia katika mji huo pamoja na magari yao 50 pia.
Wanamgambo wa Ansar Dine wameshaelezea azma yao ya kutangaza sheria ya kiislam nchini Mali huku wafuasi wa chama cha ukombozi cha AZWAD lengo lao lilikuwa kutangaza dola la watuareg,kaskazini mwa Mali.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri Yusuf Saumu