Vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi Magazetini
1 Agosti 2017Tunaanzia Marekani ambako vikwazo vya rais Donald Trump dhidi ya Urusi vinazusha wasi wasi pia katika nchi za Umoja wa ulaya. Gazeti la Allgemeine-Zeitung" linaandika: "Ikiwa Ujerumani na nchi za Umoja wa Ulaya zinaingiwa na hofu vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi visije vikaathiri pia sekta ya nishati barani Ulaya, basi hofu zao si za bure. Mabomba ya mafuta yanayopitia katika bahari ya Mashariki, kaskazini mwa Ujerumani "North Stream Pipeline" ni mradi unaosimamiwa na Ulaya na Urusi pia. Ila safari hii dhamiri mbaya haijatokana na Donald Trump bali bunge la Marekani. Ikiwa baraza la Seneti na lile la wawakilishi wanazuwia uamuzi wa rais, kawaida uamuzi wao tunauunga mkono lakini safari hii wamevuna walichokipanda."
Mada hiyo hiyo ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi imechambuliwa pia nha gazeti la "Frankenpost linaloandika: "Kitisho kimetanda kati ya ikulu ya Urusi Kremlin na ikulu ya Marekani White House. Baraza la Seneti la Marekani limepiga kura kuzidisha vikwazo dhidi ya Urusi. Moscow nayo ikajibu kwa kuwafukuza wanadiplomasia wengi kupita kiasi, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni. Kwa namna hiyo njia nyingi za mawasiliano zimevunjika na kitisho cha suitafahamu kimezidi kukuwa. Wanadiplomasia wanawajibika zaidi hasa pale viongozi wa taifa wanapozozana mfano wa kile kinachotokea wakati huu tulio nao kati ya Vladimir Putin na Donald Trump. Sasa lakini wanadiplomasia wengi wametimuliwa na hiyo yaonyesha kuwa ishara mbaya.
Kashfa ya magari ya Diesel
Mada ya pili iliyohanikiza magazetini inahusiana na kashfa inayoyagubika makampuni ya magari nchini Ujerumani. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika: "Baada ya yote watu waliyoyasikia hadi wakati huu, mafuta ya Diesel bado mustakbali wake si mbaya, tena yanaweza kuwa nishati safi itakayosaidia kusafisha mazingira tena bila ya vifaa bandia. Diesel safi ikichanganyika na injini inayoendeshwa kwa umeme ina uwezo mkubwa na inaweza kufunika mwanya hadi magari yanayoendeshwa kwa nguvu za umeme yatakapoenea. Ikiwa wakuu wa makampuni watawahimiza wahandisi wao wawajibike ipasavyo ,basi na ufumbuzi wa tatizo hautakuwa mbali kupatikana."
Baraza la katiba Venezuela
Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Venezuela na kasheshe ya kuchaguliwa baraza la katiba zoezi lililozusha machafuko na kusababisha damu kumwagika. Gazeti la mjini Cologne, Kölner Stadt Anzeiger linaandika: "Baraza hilo jipya litakutana wiki hii na tangu sasa mtu anaweza kuashiria katiba mpya ya Venezuela itakuwa ya aina gani. Itampatia rais madaraka makubwa zaidi na kulipokonya kwa namna hiyo madaraka yake bunge na taasisi za sheria. Hilo Maduro na kundi lake wamehakikisha liwe hivyo. Na katika hotuba yake ya kwanza baada ya uchaguzi, rais Maduro ameshawaonya wabunge wa upande wa upinzani na vyombo vya habari. Kuhusu uchaguzi wa magavana, ameelezea utayarifu wa kuzungumza na upande wa upinzani."
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef