1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vyafikia mwisho

18 Oktoba 2020

Vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyopiga marufuku kuiuzia au kununua silaha kutoka Iran vimefikia mwisho leo kama ilivyoafikiwa na madola yenye nguvu licha ya upinzani kutoka Marekani.

Iran Raad-500-Rakete
Picha: AFP/IRAN PRESS

Umoja wa Mataifa uliipiga marufuku Iran kununua silaha ikiwemo vifaru na ndege za kivita kutoka mataifa ya kigeni mwaka 2010 kufuatia msuguano uliozuka kuhusiana na mradi wake tata wa nyuklia. Hapo kabla umoja huo uliweka vikwazo dhidi ya mauzo ya silaha kutoka Iran.

Ingawa yenyewe inasisitiza kuwa haina mipango ya kununua silaha, kwa nadharia lakini Iran sasa inaweza kununua silaha inazotaka kuimarisha hazina yake ya  zana na mifumo ya ulinzi ambayo imekuwepo tangu mapinduzi ya kiislamu yalipofanyika mwaka 1979. Pia nchi hiyo inaweza kuuza tena zana zote za kijeshi zinazotengenezwa na kampuni za ndani.

Jamhuri hiyo ya kiislamu imeitaja hatua ya kufikia mwisho kwa vikwazo vya silaha kama "siku ya ushindi kwa jumuiya ya kimataifa .. katika kupinga juhudi za utawala wa Marekani".

"Hatua ya leo ya kurekebisha ushirikiano wa ulinzi kati ya Iran na ulimwengu ni ushindi katika mwelekeo wa mshikamano wa dunia, amani na usalama kwenye kanda yetu" ameandika waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Mohamed Javad Zarif kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Marekani inapinga hatua hiyo 

Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Imago Images/Xinhua

Hata hivyo utawala wa Rais Donald Trump umesisitiza kuwa bado vikwazo dhidi ya Iran vinafanya kazi kwa kuwa yenyewe imetengua kipengele kimoja kutoka mkataba wa nyuklia kati ya Iran na madola yenye nguvu ambao Marekani ilijiondoa mwaka 2018. Madai hayo yamepuuzwa na jumuiya ya kimataifa.

Wakala unaoshughulikia ujasusi kwa ajili ya ulinzi nchini Marekani ulitabiri kuwa iwapo vikwazo dhidi ya Iran vitafikia mwisho, nchi hiyo itajaribu kununua ndege za kivita za Urusi chapa Su-30, Yak-130 kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi na vifaru aina ya T-90.

Kadhalika serikali mjini Tehran inaweza kujaribu kununua mfumo wa ulinzi wa makombora wa S-400 kutoka Urusi pamoja na mifumo ya ulinzi mahsusi kwa ajili ya maeneo ya pwani. China pia inaweza kuizuia silaha Iran.

Kwa muda mrefu Iran imekuwa ikizidiwa uwezo na mataifa ya washirika wa Marekani kwenye eneo la ghuba mfano wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambazo zimenunua zana za kisasa za ulinzi za mabilioni ya dola kutoka Marekani.

Katika kujibu mapigo, Iran iliamua kuanza kuunda silaha zake yenyewe ikiwemo makombora ya masafa marefu.

Mvutano mkali kati ya Iran na jirani zake wa mataifa ya Ghuba

Picha: picture-alliance/dpa/U.S. Navy

Iran imeishambulia hatua ya nchi za eneo la ghuba ya kununua mifumo ya ulinzi ya Marekani  ikisema "kwa bahati mbaya ni mikataba yenye faida nyingi"  huku sehemu ya islaha hizo zikitumika katika vita vinavyoendelea nchini Yemen.

 Mzozo huu umeshuhudia muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ukiiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Iran.

Vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa havikuizuia Iran kutuma silaha tangu bunduki za rashasha hadi makombora ya masafa ya kati na marefu kwa waasi wa Houthi nchini Yemen.

Wakati Tehran inapinga kuwapatia silaha wahouthi, serikali za mataifa ya magharibi na wataalamu wa masuala ya silaha mara kadhaa wamehusisha silaha za Iran na waasi wa Yemen.

Mataifa sita ya eneo la ghuba ambayo yaliunga mkono kurefushwa kwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran walisema usafirishwaji silaha kutoka Iran kwenda Yemen kama sababu ya kupinga kuruhusiwa tena kwa serikali ya Tehran kununua silaha.

Kadhalika waorodhesha katika barua yao kwenda kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kisa cha Iran cha kuidungua kwa bahati mbaya ndege ya abiria ya shirika la ndege la Ukraine na jeshi la majini la Iran kwa kuwauwa mabaharia 19 katika shambulizi la kombora la bahati mbaya wakati wa mazoezi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW