Vikwazo vya wanawake wajasiriamali Afrika
26 Januari 2026
Mkutano huo uliwakutanisha wanawake wajasiriamali, wataalamu wa biashara, wabunifu wa teknolojia na watunga sera kutoka Afrika Mashariki. Miongoni mwa hoja kuu zilizojitokeza ni namna teknolojia ya akili mnemba (AI) inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwasaidia wanawake kuvuka vizingiti vinavyowazuia kukua kibiashara.
Wanawake wengi wajasiriamali hukosa fursa sawa za kupata ufadhili wa kibiashara. Changamoto kubwa ni ukosefu wa dhamana, hali inayowafanya washindwe kukidhi masharti magumu ya benki na taasisi nyingine za kifedha.
Ripoti za sekta zinaonyesha kuwa idadi ndogo ya biashara ndogo na za kati (MSMEs) zinazomilikiwa na wanawake hupata ufadhili rasmi ikilinganishwa na zile zinazoongozwa na wanaume. Takwimu za Taasisi ya African Times Network zinaonyesha kuwa takribani asilimia saba tu ya biashara za wanawake hupata ufadhili wa aina hiyo.
Aidha, wanawake wengi hawana mitandao imara ya wawekezaji wala ushauri wa kifedha, jambo linalowanyima fursa za kupata mtaji, kuunganishwa na wafadhili, au kujifunza mbinu za kukuza biashara zao. Ukosefu wa ufikiaji wa teknolojia za kisasa pia hupunguza uwezo wao wa kuwasiliana na wateja, kufanya masoko ya kidijitali na kupata taarifa za kifedha kama mikopo au ruzuku.
Hatua muhimu itakayowasaidia wanawake
Bernice Fernandes kutoka Tanzania, mwanzilishi wa shirika la Accelerate Women, anasema mkutano huu ni hatua ya kuziba pengo hilo. Amesema huo ni mkutano wa kwanza wa Accelerate Women East Africa Forum wenye lengo la kuwasaidia wanawake kuvuka mipaka ya biashara.
" Kaulimbiu yetu ni Mwanamke Asiyezuilika. Tunawaleta wanawake pamoja ili wajifunze, washirikiane, waunganishwe na masoko mapya, na wapate uzoefu kutoka kwa wanawake wengine wanaofanya biashara katika nchi tofauti,” alisema mwanamke huyo.
Hata hivyo, vikwazo vya kifedha bado ni changamoto kubwa. Swali linalojitokeza ni: teknolojia ya akili mnemba inaweza kusaidia vipi? Vimal anasema teknolojia ya AI inaweza kuwezesha mifumo mbadala ya tathmini ya mikopo kwa kutumia data kama miamala ya simu, malipo ya kidijitali na historia ya biashara. Hii huwasaidia wajasiriamali wanawake kupata mikopo bila kuhitaji dhamana kubwa.
Namna teknolojia ya akili mnemba (AI) inavyosaidia
Pia, majukwaa ya mafunzo yanayotumia AI yanaweza kuwasaidia wanawake kuandaa mipango ya biashara, kuelewa taratibu za maombi ya mikopo na kufanya utafiti wa soko. Mafunzo haya hubadilishwa kulingana na mahitaji ya mtumiaji, hivyo kuwa rahisi na yenye ufanisi zaidi. Mfanyabiashara na mwenyekiti wa Bidco Africa, Vimal Shah, anasema changamoto kubwa huanza pale mtu anapojizuia mwenyewe.
"AI inakupa zana zote unazohitaji, mafunzo, maarifa na hata ushauri wa kitaalamu. Hilo halihusu wanawake pekee, bali pia wanaume,” alisisitiza Shah.
Mbali na hilo, AI inaweza kusaidia kupanua masoko kwa kuunganisha wajasiriamali wanawake na washauri, wawekezaji na wafadhili sahihi. Kupitia majukwaa ya kidijitali, wanawake wanaweza kufikia masoko ya kimataifa, kuuza bidhaa mtandaoni na kujenga mitandao mipya ya kibiashara.
Zana hizi pia husaidia kufanya maamuzi ya kifedha yanayotegemea data, kama wakati sahihi wa kuwekeza, kupanua biashara au kupunguza gharama, hatua inayoongeza uendelevu wa biashara.
"Ni lazima uendane na AI. Ukijitenga nayo, itakuwa vigumu kuendelea kufanikiwa. Dunia inabadilika, na AI ni sehemu ya mabadiliko hayo,” alisema mfanyabiashara huyo.
Wanawake wanao kabiliana na changamoto hizo
Miongoni mwa wanawake waliovuka vizingiti vya kibiashara ni Maryanne Musangi, mwenyekiti wa Muungano wa Women in Manufacturing. Amefanya kazi katika sekta mbalimbali, ikiwemo benki, hoteli na viwanda, na sasa anatumia fursa za Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kupanua biashara zake.
AfCFTA, iliyoanzishwa mwaka 2018, inalenga kuunda soko moja la Afrika kwa kuondoa ushuru na kuimarisha biashara kati ya nchi wanachama, ikiunganisha zaidi ya watu bilioni 1.3 barani Afrika. Maryanne anaelezea manufaa ikiwa ni pamoja na kuendelea kukua na sasa wanahudumia masoko ya COMESA.
" Kupitia AfCFTA, tunapanua biashara barani Afrika. Januari 2026 tutaanza uzalishaji nchini Ghana kwa kushirikiana na mjasiriamali mwanamke wa huko,” alisema mwanamke huyo.
Kwa ujumla, uwekezaji katika teknolojia jumuishi na mafunzo ya akili mnemba kwa wanawake unaweza kuwa daraja muhimu la kuvuka pengo la kifedha na kijinsia.