1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vyaathiri biashara ya bidhaa za kiutu Iran

Josephat Nyiro Charo8 Agosti 2014

Chakula na dawa ni vitu ambavyo havijajumuishwa katika vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran, lakini benki nyingi zinahofia faini zinazotozwa na Marekani ijapokuwa biashara ni halali.

Medikamente in einer Apotheke im Iran
Picha: ATTA KENARE/AFP/Getty Images

Vikwazo vikilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia vinaruhusu biashara ya bidhaa kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu kama vile dawa na chakula. Lakini benki nyingi zinakwepa mikataba yoyote ya kibiashara na Iran kutokana na orodha ndefu ya faini zinazotozwa na idara husika za Marekani, kwa kujihusisha na mataifa yaliyowekewa vikwazo. Mfano mzuri wa hivi karibuni kabisa ni faini ya dola bilioni 8.97 dhidi ya benki ya BNP Paribas ya Ufaransa.

Kutoka mwezi Januari hadi Machi mwaka huu meli inayoendeshwa na Ugiriki ilitia nanga kiatika bandari moja nchini Iran kabla kulazimishwa kuelekea Fujairah katika Jumuiya ya Falme za Kiarabu kujaza mafuta, hili pia likiwa vigumu kufanyika nchini Iran kutoka na vikwazo. Hatimaye, kibali cha uuzaji wa bidhaa zilizokuwa katika meli hiyo kilitolewa na meli hiyo ikashusha shehena yake nchini Iran, lakini baada ya miezi kadhaa ya muda kupotea na gharama kubwa.

Bidhaa kwenda Iran zazuiwa

Wairan wanalalamika kuhusu hatua hizi za kutatiza biashara wakisema ndizo zilizosababisha bei ya bidhaa nchini mwao kuongezeka mno na kwepo kwa uhaba wa dawa kwa ajili ya wagonjwa kama vile wa saratani.

Bei ya vyakula imeongezeka Iran

Mashirika ya safari za meli, maafisa wa Iran na wauzaji vyakula na dawa wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba idadi inazidi kuongezeka ya shehena za bidhaa zinazoelekea nchini Iran kuzuia au kusimamishwa kabisa.

Muuzaji mmoja wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu kutoka nchini Marekani amesema sekta ya benki ndiyo inayosababisha tatizo kubwa, huku benki zikishuhudiwa zikiacha kabisa kutoa huduma zinazotakiwa kuwezesha usafirishaji wa shehena za bidhaa hizo. Muuzaji huyo aidha amesema ni vigumu kufanya biashara hiyo, gharama zimekuwa kubwa na inaonekana itakuwa vigumu zaidi kufanya biashara. Maafisa wa Marekani wamesema serikali ya mjini Washington inafahamu kuhusu tatizo hilo na inachukua hatua kurahisisha biashara ya bidhaa za kiutu.

Wairan wote wanaumia

Vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya vinawaumiza Wairan waliokuwemo na wasiokuwemo; wale waliolengwa kwa kuhusika na mpango wa nyuklia na wananchi wa kawaida ambao hawana walijualo kuhusu suala hilo. Maisha kwao yamekuwa magumu na yanazidi kuwa magumu kila kuchao.

Dawa hazipatikani kiurahisi IranPicha: Getty Images/AFP

Babak Saremi, mwalimu mwenye umri wa miaka 43 anaugua ugonjwa wa damu na anahitaji kufanyiwa matibabu mara moja kwa mwezi yanayogharimu rial milioni 4.5. Anasema mshahara wake ni dola 300 kwa mwezi, ameshauza gari yake, na mke wake ametumia vipande kadhaa vya dhahabu kulipia gharama zake za matibabu, lakini bei ya dawa kwa ajili ya matibabu hayo inazidi kuongezeka na ni vigumu dawa zenyewe kupatikana.

Fundi kinyozi Faranak Mirzaie mwenye umri wa miaka 27 amesema katika miaka saba iliyopita amelazimika kuwatafuta wafanyabiashara katika soko lisilo rasmi mjini Tehran kununua dawa kwa ajili ya mama yake anayeugua saratani. Anasema tangu Januari mwaka huu imekuwa vigumu kupata dawa za saratani kwenye hospitali zinazoendeshwa na serikali na hata katika maduka ya kuuza dawa.

Kampuni moja ya Marekani inayoiuzia Iran vifaa vya utabibu imesema huchukua miezi kadhaa kupata kibali kwa kuwa benki chache sana hukubali barua ya mkopo kutoka kwa Iran. Na hata zikikubali huchukua miezi kadhaa kabla kuweza kufanya chochote,ajambo ambalo ni changamoto kubwa hasa kama bidhaa zimeshasafirishwa kwa meli.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW