Vilabu vya Bundesliga vyajinoa kuanza upya
24 Julai 2017Vilabu vya Bundesliga vimeingia kambini kujinoa kwa msimu ujao , ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich bado wako katika ziara barni Asia ambako wamekwisha cheza michezo miwili, ambapo waliangukia pua , baada ya kushindwa na Arsenal London katika mchezo ambao uliamuliwa kwa mikwaju ya penalti 3-2 na kisha kupata kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya AC Milan.
Kesho Jumanne Bayern inaingia uwanjani kujaribu bahati yake katika ziara hiyo kwa kupambana na kikosi cha kocha Antonio Conte , Chelsea ambacho kimeongezwa makali kwa kumpata mshambuliaji Alvaro Morata kutoka Real Madrid ya Uhispania. Kocha Carlo Anceloti hata hivyo anasema hana wasi wasi ama presha licha ya timu yake kusuasua katika michezo ya majaribio. Amesema " iwapo atakuwa na presha wakati huu , basi msimu utakapoanza atakuwa amekufa." Bayern inacheza pia na Inter Milan siku ya Alhamis.
Makamu bingwa RB Leipzig tayari iko kambini na imejiimarisha kwa kuwasajili baadhi ya wachezaji chipukizi kadhaa pamoja na kuwabakisha kikosini wachezaji wake muhimu kama Naby Keita ambaye anasakwa na Liverpool ya Uingereza kwa kitita hadi euro milioni 80. Hata hivyo viongozi wa Leipzig wamesema hawana wazo la kumuuza Naby Keita, ama mchezaji mwingine wa kati Emil Forsberg.
Borussia Dortmund ilimaliza ziara yake ya bara la Asia wiki iliyopita na inaingia kambini rasmi tarehe 26 mwezi huu, nchini Uswisi, huku ikikabiliwa na tetesi za mshambuliaji wake hatari Pierre Emerick Aubamiyang kuipa mkono wa kwaheri klabu hiyo majira ya baridi msimu ujao. Lakini mkurugenzi wa sporti wa BVB Michael Zorc amewahakikishia mashabiki wa klabu hiyo kuwa Auba haendi kokote msimu ujao.
Pia mchezaji wa ulinzi Sokrates amehusishwa na uhamisho kwenda Juventus Turin ya Italia, baada ya klabu hiyo bingwa ya Italia kumpoteza mlinzi wake muhimu Bonuci ambaye katimkia kwa mahasimu wao AC Milan. Schalke 04 pia nayo imo katika ziara barani Asia na ilitoka sare ya bao 1-1 na Inter Milan ya Italia wiki iliyopita. Ligi ya Ujerumani Bundesliga inaanza rasmi tarehe 18 Agosti ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich itakwaana na Bayer Leverkusen.
Mchezaji bora wa mwaka
Wakati huo huo Philip Lahm ambaye amekuwa mlinzi imara wa kulia wa klabu ya Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani Die Mannschaft , na kutundika madaluga yake msimu uliopita akiwa nahodha wa Bayern , ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka na jopo la waandishi habari za michezo wa Ujerumani. Kocha bora msimu uliopita ni Julian Nagelsmann wa Hoffenheim ambaye ameiweka timu hiyo katika nafasi ya nne msimu uliopita na kuonja kucheza katika Champions League msimu ujao.
Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB linakabiliwa na malipo ya kodi ya euro milioni 26 kutokana na uchunguzi kuhusiana na malipo yaliyofanywa katika fainali za kombe la dunia mwaka 2006.
Katika ripoti yake ya mwisho kwa mwaka 2016 , DFB imesema imefahamishwa na mamlaka ya kodi kuhusiana na mabadiliko ya tathmini ya kodi kwa mwaka 2006 baada ya shirikisho hilo kusema halikupata faida kwa mwaka huo na tathmini hiyo kukataliwa. Kutokana na hilo shirikisho la kandanda nchini Ujerumani DFB litalazimika kulipa kiasi cha euro milioni 26, imesema ripoti ya fedha. Hata hivyo DFB inaamini kwamba uamuzi huo utabadilishwa baada ya kukata rufaa.
Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wanatarajia kumtangaza mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo katika muda wa wiki sita na kufikisha mwisho mwaka mzima ambapo nafasi hiyo ilikuwa wazi, amesema rais wa klabu hiyo Uli Hoeness leo Jumatatu. Nafasi hiyo ilikuwa wazi tangu Matthias Sammer kujiondoa mwaka mmoja uliopita. Nahodha wa zamani wa Bayern Philipp Lahm alionekana kuwa mmoja wa watu wanaoweza kuchukua wadhifa huo lakini alikataa, na Hoeness hakutaka kuzungumzia iwapo mlinda mlango wa zamani wa Bayern Oliver Kahn ni mmoja wa watu wanaowania nafasi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Yusuf , Saumu