Vilabu vya Bundesliga vyarejea mazoezini
6 Aprili 2020Kandanda limesimama kwa karibu mwezi sasa na kitengo kinachosimamia ligi ya Ujerumani DFL kimesema marufuku hiyo itaendelea kutekelezwa hadi angalau Aprili 30.
Vilabu hata hivyo vimepewa ruhusa ya kuanza mazoezi wiki hii, huku wachezaji wa mabingwa Bayern Munich, Borussia Moenchengladbach, VfL Wolfsburg, Eintracht Frankfurt, Paderborn na wengine wakiamua kufanya mazoezi katika vikundi vidogo vidogo ili kupunguza maambukizi.
Lakini vilabu kama Bayern vikirejea mazoezini, kuna vingine kama Werder Bremen ambavyo vimeshindwa kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu mji wa Bremen haujaondoa vizuizi vilivyowekwa vya kuwataka watu kuepuka mikusanyiko. Kocha wa Werder Florian Kohfeldt amesema kuwa wataendelea kutekeleza hatua hizo, ijapokuwa wanahofia kuwa hali hiyo huenda ikaathiri juhudi zao za kuepuka kushushwa daraja.
Bremen wapo katika nafasi ya pili ya mkia kwenye msimamo wa Bundesliga, na pointi nne juu mbele ya Fortuna Duesseldorf.
Kitendawili hata hivyo ni lini Bundesliga itarejea kutimua vumbi?
Kipa wa zamani wa Ujerumani Rene Adler anahofia kuwa kutakuwa na mtazamo hasi kutoka maeneo mengine ya jamii kama Bundesliga itaruhusiwa kuendelea na mechi zilizosalia katika wakati huu wa janga la virusi vya corona.
Adler ameliambia toleo la leo la jarida la michezo la Ujerumani, Kicker kuwa Ujerumani huenda ikaleta tatizo katika jamii kama kandanda litaruhusiwa kuendelea na shughuli nyingine zifungiwe. Adler anasema hatua hiyo huenda ikaleta ukosefu wa usawa ikilinganishwa na sekta nyingine za kiviwanda ambazo pia hazina mapato kutokana na hatua za serikali kusitisha shughuli zote na sasa zinajitahidi kukabiliana na hali hiyo.