1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vilabu vyarejea mazoezini kabla ya kuanza mzunguko wa pili

6 Januari 2025

Baada ya mapumziko mafupi ya msimu wa baridi kali vilabu vya ligi kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga vimerejea mazoezini kwa ajili ya kuanza mzunguko wa pili wa msimu.

Beki wa Bayern Kim Min Jae akiwa mazoezini
Vinara Bayern Munich watalenga kuendeleza ubabe wao kileleni katika BundesligaPicha: Bernd Feil/M.i.S./IMAGO

Vinara Bayern Munich walianza maandalizi yao huku wakimkaribisha nahodha wao Manuel Neuer. Baada ya kuumia mbavu mwanzoni mwa Desemba, kipa huyo wa zamani alirejea katika mazoezi ya kikosi cha kwanza chini ya kocha Vincent Kompany. Wengine walioshiriki ni Harry Kane, Jamal Musiala, Joshua Kimmich na Thomas Mueller. Watacheza Jumatatu mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Austria Salzburg na kisha kurejea dimbani Jumamosi ijayo dhidi ya Borussia Moenchengladbach.

Soma pia: Bayern mabingwa wa mzunguko wa kwanza wa msimu wa Bundesliga

RB Leipzig nao walianza mwaka mpya kwa tabasamu baada ya kumkaribisha mazoezini kiungo mchezeshaji Xavi Simons. Mholanzi huyo alijeruhiwa kifundo cha mguu mwishoni mwa Oktoba, amerudi kikosini kwa mara ya kwanza. Beki ya kushoto David Raum pia amerejea kutoka mkekani. Leipzig ambao ni wa nne kwenye msimamo wa ligi, watarejea dimbani Januari 12 dhidi ya Werder Bremen

Habari mbaya kwa mabingwa watetezi Bayer Leverkusen ni kuwa watalazimika kukosa huduma za mshambuliaji aliyeumia Victor Boniface kwa muda mrefu kuliko ilivyodhaniwa kabla. Kurejea kwake kumecheleweshwa kutokana na tatizo dogo katika mpango wake wa matibabu. Mnigeria huyo mwenye umri wa miaka 24, alitarajiwa kurejea mazoezini mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kuumia misuli ya paja. Hajaichezea Leverkusen tangu Novemba 9.

Uhamisho wa Januari

Wakati huo huo, dili za kwanza za Bundesliga katika dirisha la uhamisho wa Januari zimeanza kupigwa. Kumekuwa na kuwa Winga wa Borussia Dortmund, Donyell Malen anawindwa na Aston Villa. Winga huyo mwenye umri wa miaka 25 alijiunga na Dortmund akitokea PSV Eindhoven mwaka wa 2021 na ana mkataba hadi 2026. Lakini ameshindwa kupata nafasi ya kucheza chini ya Kocha Nuri Sahin.

Biashara imejikokota mpaka sasa, ijapokuwa mabingwa Leverkusen tayari wamemsaini mshambuliaji wa Kiargentina mwenye umri wa miaka 18, Alejo Sarco kutoka klabu ya CA Velez Sarsfield hadi mwaka wa 2029.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW