1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vilio na simanzi wakati wa kuagwa mwili wa Hayati Magufuli

20 Machi 2021

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewaongoza viongozi mbalimbali, wakiwemo wabunge, mawaziri na wananchi, kumuaga aliyekuwa Rais wa Taifa hilo John Pombe Magufuli aliyefariki Machi 17.

Tansania | Beisetzung Präsident John Magufuli in Dar es Salaam
Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amewaongoza viongozi mbalimbali, wakiwemo wabunge, mawaziri na wananchi, kumuaga aliyekuwa Rais wa Taifa hilo John Pombe Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu, jijini Dar es alaam kutokana na tatizo la mfumo wa umeme kwenye moyo.
Rais Suluhu ambae ameapishwa kushika wadhifa huo hapo jana baada ya kifo cha mtangulizi wake dokta John Magufuli, macho yake yalionekana kudhoofika na kuchoka aliketi mita chache kutoka lilipokuwa jeneza la hayati Magufuli na mjane wake Janeth Magufuli.

Vilio na majonzi vilitawala katika uwanja wa Uhuru, ambapo shughuli ya kutoa heshima ya mwisho kwa kiongozi huyo alieonekana kuwa na misismamo ya kujitegemea kiuchumi zilifanyika huku baadhi ya wananchi wakibeba mabango mbalimbali ambayo baadhi yalisomeka “ Chuma cha Afrika kimedondo.” Awali kabla ya zoezi la kuuaga mwili wa Magufuli, kulitanguliwa na ibada ya misa takatifu  katika kanisa la Mtakatifu Petro. 

RUWA’ICH: SULUHU ANAIJUA NCHI ATENDE HAKI

Wanajeshi wakisindikiza mwili wa hayati Magufuli Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Misa takatifu ya kuaga mwili wa Rais Dokta John Magufuli aliyefariki akiwa na umri wa miaka 61, imeongozwa na Askofu mkuu wakanisa katoliki jimbo kuu la Dar es salaam Yuda Taddeus Ruwa’Ich, pamoja na askofu mkuu mstaafu mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na katibu mkuu wa askofu baraza kuu la Tanzania ( TEC ) Father Charles Kitima.
Katika ibada ya misa hiyo maalum, Askofu Ruwa’ich, anamzungumzia Rais Magufuli kama mtu aliependa kutenda haki kwa kila tabaka la watu, hivyo kulitolea mwito taifa kuja pamoja katika kipindi hiki alichokitaja ni kigumu kwa taifa.

“Tunapomuombea Hayati John Magufuli napenda kuwaalika tuliombee pia taifa hili ambalo alilipenda na kulihudumia kwa nguvu zake zote, kusudi taifa liendelee kuwa na umoja, liendelee kujituma, liendelee na utawala wa haki, kushughulikia usawa utu na maendeleo ya raia Wake.” Alisema askofu Ruwa’Ich.

Akiugeukia utawala mpya na wa kihistoria chini ya mwanamke anayeonekana mwenye haiba ya upole na unyenyekevu, Rais Samiha Suluhu, ameutazama wadhifa wa urais si kazi rahisi, kwani umebeba jukumu la kuwahudumia wananchi kwa usawa.“Samia anaifahamu nchi, anajua vipaumbele vyake na kuyaendeleza kwa juhudi mema yalioshughulikiwa na hayati Magufuli.” Alisisitiza Askofu Ruwa’Ich huku akimtazama Rais Suluhu.

MAELFU WAJITOKEZA BARABARANI KUUAGA MWILI WA MAGUFULI

Maelfu ya waombolezaji wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania John MagufuliPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Maelfu ya Waombolezaji walijitokeza barabarani kutoa heshima zao za mwisho kwa jemedari wa taifa hilo, wakati mwili wake ulipotoka katika kanisa la S.t Peters Oystabay hadi katika uwanja wa uhuru Dar es salaam. Vilio vya majonzi vilisikika kando mwa barabara ambapo msafara uliobeba mwili wa marehemu Rais Magufuli ulipita, baadhi ya watu walimwaga maua, wengine walivua khanga na mashati yao kuyatandika chini ikiwa ni ishara ya kuomboleza msiba wa kiongozi huyo aliyefariki akiwa mamlakani kwa muda wa miaka 5, na baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa mwaka 2020, alikuwa ameanza kutumikia awamu yake ya pili ya miaka mitano na ya mwisho kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mwili wa Rais Magufuli unatarajiwa kuagwa kwa siku mbili katika jiji la Dar es salaam Machi 20 na Machi 21 na kisha Dodoma Machi 22 ambapo utaagwa na viongozi wa mataifa mbalimbali, wawakilishi wa kidiplomasia na wananchi wa mikoa ya kanda ya kati. Machi 23 wananchi wa Zanzibar wataongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi kutoa heshima za mwisho na baada ya hapo Machi 24 wananchi wa Mwanza mkoa ambao enzi za uhai wake Rais Magufuli alitumia muda mrefu kwa makaazi.Matumaini ya Wazanzibari katika urais wa Samia Suluhu Hassan

Wananchi wa mkoa wa Geita watapata fursa ya kumuaga mpendwa wao nyumbani kwao Chato na mnamo Machi 26 shughuli za mazishi zitafanyika mbapo siku hiyo imetangazwa na serikali kama ni siku ya mapumziko ili wananchi wote washuhudie maziko ya Rais huyo, aliejipambanua kuwatetea wananchi wa hali ya chini.

Wakati huo huo, kamati Kuu ya chama tawala nchini Tanzania,(CCM) itakutana leo Jumamosi jijini Dar es salaam, kujadili agenda ambazo bado hazijawekwa wazi. Kikao hicho kinafanyika siku moja tu baada ya taifa hilo kumpata Rais Mpya, Samia Suluhu Hassan aliyeapishwa jana Ijumaa baada ya mtangulizi wake, John Magufuli kufariki dunia wiki hii. Na kitendawili kinachosalia sasa ni kuhusu nani atakuwa Makamu Mpya wa Rais. 
Tayari Spika wa Bunge Job Ndugai amewaita wabunge wote kwenda Dodoma ambako pamoja na mambo mengine wanatarajiwa kuidhinisha jina la makamu wa rais kwa idadi ya kura zisizopungua asilimia 50 ya wabunge wote.

Mwandishi: Hawa Bihoga dw Dar es salaam
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW