1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Viongozi duniani wampongeza Erdogan

29 Mei 2023

Viongozi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa Uturuki Recep Tayipp Erdogan, baada ya kushinda katika duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika Jumapili, ambapo ametoa wito wa mshikamano wa kitaifa.

Türkischer Präsident Rcep Tayyip Erdogan | Ankara, Türkei
Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Katika duru ya pili ya uchaguzi, Erdogan alimshinda mpinzani wake Kemal Kilicdaroglu kwa kupata asilimia 52.14 ya kura, huku Kilicdaroglu akipata asilimia 47.9.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi na Baraza Kuu la Uchaguzi, Erdogan amesema sasa ni wakati wa kuweka kando tofauti zozote zilizojitokeza wakati wa uchaguzi na kuungana, ili kujumuisha malengo yao ya kitaifa na ndoto za taifa hilo.

"Mshindi ni Uturuki, mshindi ni taifa letu na makundi yake yote, demokrasia yetu ndiyo imeshinda. Hakuna aliyeshindwa leo, raia wote milioni 85 wameshinda," alifafanua Erdogan.

Pongezi za viongozi ulimwenguni

Miongoni mwa viongozi waliompongeza Erdogan ni Rais wa Marekani, Joe Biden na Rais wa Urusi, Vladmir Putin. Katika ukurasa wake wa Twitter, Biden ameandika kuwa anatarajia wataendelea kufanya kazi pamoja na Erdogan na kushirikiana kama washirika wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, katika kushughulikia changamoto za ulimwengu.

Putin ambaye amekuwa akishirikiana kwa karibu na Erdogan katika masuala muhimu ya kimataifa, licha ya kutofautiana kwenye masuala kadhaa, amesema ushindi wake umetokana na kujitoa kwake kama kiongozi wa wananchi wa Uturuki. Amesema huo ni ushindi wa wazi kwamba Waturuki wanaunga mkono juhudi zake za kuimarisha mamlaka ya serikali na kufuata sera huru za kigeni.

Wananchi wa Uturuki mjini Istanbulwakishangilia ushindi wa Rais Recep Tayyip Erdogan Picha: Emrah Gurel/AP Photo/picture alliance

Aidha, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amempongeza rais huyo kwa kuchaguliwa tena na kusema kwamba umoja huo unataka kuimarisha uhusiano wake na Uturuki.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amesema anatazamia kuendelea kushirikiana na Erdogan na kuandaa mkutano wa kilele wa muungano huo wa kijeshi utakaofanyika mwezi Julai.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema anatazamia kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Uturuki na umoja huo.

Scholz asifu ushirikiano wa Ujerumani na Uturuki

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amepongeza ushindi wa Erdogan kwa kusifu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ambapo amesema watu na uchumi wao umeingiliana sana. Scholz amesema kwa pamoja wanataka kuendeleza ajenda yao ya pamoja kwa msukumo mpya.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amempongeza Erdogan kwa ushindi wake akisema tangu Urusi ilipoivamia Ukraine amekuwa akijiweka kama mpatanishi wa mzozo kati ya Ukraine na Urusi.

Viongozi wengine waliompongeza Erdogan ni Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed al-Nahyan, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, Kaimu Waziri Mkuu wa Afghanistan Al-Haj Mullah Muhammad Hassan Akhund, pamoja na China.

 

(AFP, DPA)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW