1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi duniani waomboleza kifo cha Rais Deby wa Chad

Sylvia Mwehozi
21 Aprili 2021

Viongozi wa ulimwengu wameendelea kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha rais wa Chad, Idriss Deby Itno aliyekuwa mshirika muhimu wa mataifa ya magharibi katika mapambano dhidi ya waasi katika ukanda wa Sahel. 

Todesfall Präsident des Tschad Idriss Deby gestorben
Picha: Ludovic Marin/AP/picture alliance

Salamu za pole zimeendelea kumiminika kufuatia kifo cha rais Deby ambapo wizara ya mambo ya nje ya Marekani imelaani "vurugu za hivi karibuni na kifo" katika taifa hilo. Kwenye taarifa yake, Marekani imesema iko tayari kuunga mkono makabidhiano ya amani ya madaraka kulingana na katiba ya Chad.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, naye ameelezea "kusikitishwa" kwake na kifo cha Deby, akimuelezea kama "mshirika muhimu hususan katika juhudi za kupambana na ugaidi, itikadi kali na uhalifu katika eneo la Sahel".

Ofisi ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nayo imetoa salamu za pole ikisema kwamba "Chad imempoteza kiongozi mkubwa na rais ambaye alifanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya usalama wa nchi na utulivu wa kikanda kwa miongo mitatu, ikimsifu pia kama rafiki wa Ufaransa "mwenye uthubutu".

Seidick Abba ambaye ni mchambuzi kuhusu masuala ya Chad anagusia uhusiano wa Ufaransa na Chad, "nina uhakika kuwa Ufaransa inajali leo kwa sababu ilihusika na Déby. Haikutetea uhuru na demokrasia nchini Chad kwani Déby alikuwa mshirika asiyeepukika. Leo Déby ametoweka na Ufaransa haijatetea uhuru. Hatukusikia kutoka Ufaransa wakati mtandao ulipofungwa nchini Chad, wakati watu walipokamatwa na wakati vyama vikuu vya upinzani vilipojiondoa kwenye uchaguzi wa urais. Kufuatia kifo cha Déby, ninaamini kwamba Ufaransa ina wasiwasi juu ya mwendelezo wa mapambano dhidi ya ugaidi".

Naye Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema tangazo la uongozi wa mpito ni lazima lifanyike katika hali ya amani, na kwa kuheshimu haki za binadamu na misingi ya uhuru sambamba na kuruhusu kuandaliwa kwa uchaguzi mpya utakaokuwa jumuishi.

Mahamat Idriss Déby Itno (katikati) aliyeteuliwa na jeshi kuiongoza kwa muda ChadPicha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Umoja wa Afrika kupitia mkuu wake Moussa Faki Mahamat, ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Chad, amesema kwamba amepokea taarifa za kifo cha Deby kwa "mshtuko mkubwa na majonzi mazito".

Katika nchi jirani ya Mali ambako pia imo katika lindi la utawala wa kijeshi, rais wa mpito Bah Ndaw ameelezea "huzuni kubwa" juu ya habari ya kifo cha kinyama cha Deby.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ametuma salamu za rambirambi kupitia ukurasa wa Twitter akimsifu Deby kama "kiongozi shupavu na haswa uamuzi wake wa kihistoria wa kufufua uhusiano wa Chad na Israel".Mahamat Deby, jenerali wa nyota nne aliyechukuwa urais wa Chad

Wakati huohuo waasi katika nchi hiyo wameapa kuudhibiti mji mkuu wa nchi katika kile kinachoweza kuwa machafuko makubwa ya kudhibiti taifa hilo la afrika ya kati lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Katika taarifa yake waasi hao wamesema "Chad sio nchi ya kifalme" wakiapa kupambana kuuchukua mji mkuu.

"Vikosi vya jeshi la Front for change and concord vinaelekea N'Djamena wakati huu. Kwa kujiamini na ujasiri mkubwa", ilisema taarifa ya waasi iliyotolewa Jumanne jioni.

Mazingira ya kifo cha Deby bado yamesalia kuwa na utata, huku wafuatiliaji wa mambo wakihoji uharaka wa jeshi kukabidhi madaraka kwa mtoto wa rais badala ya kufuata katiba na kuibua wasiwasi wa kutokea machafuko.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW