Viongozi duniani wazungumzia mwaka mmoja wa vita Ukraine
24 Februari 2023Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesema Waukraine watashinda pasina shaka katika vita vyao dhidi ya Urusi na kuongeza kuwa uhuru laazima upiganiwe kila siku.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, amesema Rais wa Urusi Vladmir Putin ameshindwa kufanikisha hata lengo moja, huku Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, akisema viongozi wa kundi la mataifa saba tajiri duniani wanaokutana baadae hii leo G7, watatoa wito kwa mataifa kutotuma msaada wa kijeshi kwa Urusi.
Marekani imetangaza vikwazo vikubwa vinavyolenga kuongeza maumivu ya kiuchumi dhidi ya Urusi, ambavyo kwa mujibu wa ikulu ya White House, vitalenga sekta za benki, madini na ulinzi. Mfalme wa Uingereza Charles III pia amelaani uvamizi wa Urusi aliosema haukuwa na sababu. Naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesisitiza msimamo wa Ufaransa kuhusu kuisaidia Ukraine.