1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi kuharakisha mchakato wa uchaguzi Somalia

Angela Mdungu
22 Oktoba 2021

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed na waziri mkuu wake Hussein Roble wamekubaliana kuharakisha mchakato wa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu na hivyo kumaliza mzozo wa muda mrefu

Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed | Farmajo
Picha: Str/AFP

Viongozi hao wawili wa Somalia walikuwa na mfarakano kuhusu teuzi za juu za nafasi za usalama, mzozo ambao uliibua hofu kuhusu utulivu wa nchi hiyo, na kuzuia juhudi za kukabiliana na wanamgambo wenye itikadi kali. Hata hivyo kauli ya pamoja ya Rais Abdullahi Mohamed na waziri mkuu Hussein Roble imesema wamekubaliana kuuharakisha mchakato huo wa uchaguzi kwa kuyataka majimbo yaitishe uchaguzi wa mabunge ya majimbo katika wiki chache zijazo.

Msuguano wa madaraka kati ya viongozi hao wawili ulibainika hadharani mwezi Septemba baada ya waziri mkuu kumfukuza mkuu wa shirika ujasusi wa Somalia kutokana na namna alivyoshughulikia kesi iliyovuta hisia za wengi ya kutoweka kwa afisa wa shirika hilo la ujasusi.

Rais Abdullahi Mohamed aliubatilisha uamuzi wa waziri mkuu kwa kumteua mkuu huyo wa ujasusi kama mshauri wake wa masuala ya usalama na akatangaza kumwondolea Roble mamlaka yake ya kiutendaji hadi mchakato wa uchaguzi utakapokamilika. kwa upande wake waziri mkuu Roble alimtuhumu Rais kwa kutaka kuhujumu utendaji wa serikali.

Ahadi ya kuacha kuzozana

Jana Alhamisi wawili hao walisema kuwa wangeacha kuzozana kuhusu teuzi na kuanza kuunga mkono uchunguzi wa mahakama kuhusu kutoweka kwa mpelelezi Ikran Tahlil ambaye familia yake imekuwa ikiwatuhumu waajiri wake kwa kumuuwa. Katika kauli yao ya pamoja viongozi hao wa Somalia walisema uongozi umekubaliana kuziacha taasisi za mahakama jukumu la kesi ya Ikran Tahlil na kuviagiza vyombo vya usalama kuuisaidia mahakama katika uchunguzi.

Somalia imekuwa ikipambana kufanya uchaguzi kwa miezi kadhaa sasa. Mamlaka ya miaka minne ya Rais Abdullahi Mohamed ilikoma mwezi Februari mwaka huu, lakini aliongezewa muda na bunge mwezi wa nne hatua iliyosababisha mapigano mjini Mogadishu huku mahasimu wake wakichukulia uamuzi huo kuwa ni kujinyakulia kwa nguvu madaraka. 

Waziri mkuu wa Somalia Hussein RoblePicha: Sadak Mohamed/AA/picture alliance

Waziri mkuu Roble aliandaa ratiba mpya ya kura, lakini mchakato huo umekuwa nyuma ya ratiba, na mwezi uliopita alimtuhumu Rais Abdullahi Mohamed kwa kuuzuia. Chaguzi nchini Somalia zinafuata mfumo mpana usio wa moja kwa moja ambapo mabunge ya majimbo na wajumbe wa koo huwachagua wabunge wa bunge la taifa ambao ndiyo wanaomchagua Rais.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW