Viongozi kutia saini makubaliano ya DRC
24 Februari 2013Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon amewaalika marais 11 katika tukio hilo la kutiwa saini kwa kile kinachojulikana kama makubaliano ya mfumo wa amani, ikiwa ni juhudi za kufikisha mwisho mzozo huo, lakini bila kuwa na maelezo maalum. Makubaliano hayo yatatiwa saini katika makao makuu ya umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Iwapo yatafanikiwa makubaliano hayo yanaweza kusababisha kuundwa kwa kikosi maalum cha jeshi la umoja wa mataifa kitakachoweza kuingilia kati , katika eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kupambana na waasi pamoja na juhudi mpya za kisiasa.
Viongozi waalikwa
Msemaji wa umoja wa mataifa Martin Nesirky amesema kuwa viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Angola, Burundi, jamhuri ya Afrika ya kati , Jamhuri ya Congo, Rwanda, Afrika kusini , Sudan ya kusini, Tanzania, Uganda na Zambia wamealikwa.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika , mataifa 11 ya mkutano wa kimataifa kuhusu eneo la maziwa makuu , (ICGLR) pamoja na jumuiya ya wanachama 14 ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, watakuwa "wadhamini wenza", amesema Nesirky. Juhudi za hapo awali za kufitiwa saini kwa makubaliano hayo mwezi uliopita zilisitishwa katika dakika za mwisho.
"Marais wote walioalikwa wamekubali ama kuhudhuria ama kutoa mamlaka ya kutia saini," taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa siku ya Ijumaa ilisema. Umoja wa Mataifa unatarajiwa kumteua mjumbe maalum kuangalia utekelezwaji wa makubaliano hayo. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa hali ya kutokubaliana mwezi Januari ilitokana na wasi wasi juu ya utaratibu, lakini sio kutokana na muktadha wa makubaliano hayo.
Makubaliano hayaeleweki
Jason Stearns, mchambuzi binafsi ambaye hufuatilia masuala ya Kamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mapema mwezi huu ameyaita makubaliano hayo kuwa ni "waraka usioeleweka kabisa, wenye kurasa mbili."
Makubaliano hayo, amesema, yanalenga katika vipengee vitatu: "kuzuwia mataifa ya eneo hilo kuingilia masuala ya ndani ya kila nchi, kuhimiza kufanyiwa mageuzi taasisi dhaifu nchini Congo na kuvutia hali bora zaidi kwa wafadhili na uhusishwaji.
Eneo la mashariki ya Kongo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini limeharibiwa na makubdi kadha yenye silaha katika muda wa miongo miwili iliyopita, huku makundi mapya ya waasi yakizuka kila mara, baadhi yao yakiungwa mkono kutoka katika nchi jirani.
Ongezeko la hivi karibuni la machafuko lilitokea mwaka 2012 na kusababisha kuzuka kwa kundi la waasi la Machi 23, (M23) ambalo kwa muda lilikamata mji muhimu wa Goma Novemba mwaka jana. M23 liliundwa na wapiganaji wa zamani wa kundi la waasi wa kabila la Watutsi, ambao wanachama wake waliingizwa katika jeshi la kawaida la serikali ya Congo chini ya makubaliano ya amani ambapo masharti yake wanadai hayakutimizwa.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga