1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia walaani shambulio dhidi ya Trump

15 Julai 2024

Viongozi mbalimbali duniani wamelaani jaribio la mauaji dhidi ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump. Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden, amesema kuwa matukio ya aina hiyo hayana nafasi katika taifa hilo.

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump akiwa kwenye kampeni huko Butler
Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump akiwa kwenye kampeni huko ButlerPicha: Gene J. Puskar/AP Photo/picture alliance

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujjaric amelaani na kuliita tukio hilo kuwa ni vurugu za kisiasa. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekitaja kitendo hicho kuwa cha chuki, wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akimtakia Trump nafuu ya haraka.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema amefedheheshwa na kushtushwa na kilichotokea na ametuma salamu za pole kwa  walioathiriwa katika tukio hilo.

Miongoni mwa  viongozi wengine waliolaani tukio hilo na kutoa pole kwa Trump  ni pamoja na Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Fumio Kishida wa Japan, Narendra Modi wa India na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Viongozi wa mataifa mengine kama Argentina, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Pakistan, Slovakia, Misri, Australia, Korea Kusini, Brazil, Uholanzi, Poland, Ugiriki, Sweden, Taiwan, Qatar, Bahrain, Palestina, Thailand, wamelaani pia tukio hilo.

Urusi yautupia lawama utawala wa rais Joe Biden

Polisi wa Marekani wakizuia barabara huko Pennsylvania karibu na makazi ya Thomas Matthew Crooks inayeaminika ndiye aliyejaribu kumuua TrumpPicha: Kyle Mazza/Anadolu/picture alliance

Ikulu ya Kremlin imesema siku ya Jumapili kwamba haiamini kuwa utawala wa sasa wa Marekani umehusika katika jaribio la Jumamosi la kutaka kumuua mgombea urais Donald Trump, lakini ulibuni mazingira ambayo yamechochea shambulio hilo.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema Urusi inalaani aina zozote za vurugu wakati wa ushindani wa kisiasa. Kauli ya Urusi imetolewa huku baadhi ya wafuasi wa Trump kutoka chama chake cha Republican wakiushutumu utawala wa Biden kuhusika na tukio hilo.

Trump alipigwa risasi sikioni wakati wa kampeni yake ya uchaguzi huko Pennsylvania, shambulio ambalo kwa sasa linachunguzwa na shirika la upelelezi la Marekani (FBI) kama jaribio la mauaji. Maafisa wamesema hadi sasa hawajafahamu dhamira ya mshambuliaji huyo ambaye aliuawa kwa risasi.

Kauli kutoka kwa Trump na wanasiasa wengine nchini Marekani

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump baada ya kujeruhiwa kwa risasiPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Mgombea urais nchini Marekani Donald Trump amesema ni Mungu pekee ndiye aliyezuia jambo lisilofikirika na kuongeza kuwa: " Ninataka kuwashukuru maafisa wa idara ya Ujasusi na maafisa wote wa usalama kwa hatua zao za haraka wakati wa shambulio la huko Butler, Pennsylvania. Muhimu zaidi, nataka kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia ya mtu aliyeuawa, na pia kwa familia ya mwingine aliyejeruhiwa vibaya. Ni ajabu kwamba kitendo kama hiki kinaweza kufanyika katika nchi yetu. Nilipigwa risasi iliyopenya sehemu ya juu ya sikio langu la kulia. Nilijua mara moja kwamba mambo si mazuri, niliposikia milio ya risasi na mara nikahisi risasi ikipenyeza kwenye ngozi. Nilitokwa na damu nyingi, kwa hivyo nikagundua ni nini kilikuwa kikiendelea. MUNGU IBARIKI MAREKANI!"

Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden amesema wanatakiwa kuungana kama taifa moja ili kulaani kitendo hicho ambacho amesisitiza kuwa hakina nafasi katika taifa hilo. Biden amesema pia kuwa anashukuru kuona Trump yuko salama na anaendelea vizuri.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amesema kwa pamoja ni lazima walaani kitendo hicho cha kuchukiza na kwamba amefarijika kusikia kuwa  Trump hajajeruhiwa sana  na kwamba wanamuombea yeye na familia yake pamoja na wote waliojeruhiwa na kuathirika na tukio hilo.

Spika wa Bunge la Marekani kutoka chama cha Republican Mike Johnson amesema anamuombea Rais Trump na wote waliohudhuria mkutano wa kampeni huko Pennsylvania, huku akiwashukuru maafisa wa usalama kwa hatua zao za kumlinda Trump. Johnson amesema kitendo hiki cha kutisha kinachodhihirisha vurugu za kisiasa kwenye mkutano wa kampeni wa amani hakina nafasi katika nchi hiyo na kinapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na kwa kauli moja.

FBI yachunguza jaribio la mauji dhidi ya Trump

Shirika la Upelelezi la Marekani linachunguza jaribio la mauaji lililomlenga siku ya Jumamosi Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump. Tukio hilo lilifanyika Jumamosi wakati Trump alipokuwa akifanya mkutano wa hadhara katika jimbo la Pennsylvania. Mtu mmoja alifyatua risasi kadhaa na kumjeruhi sikioni Rais huyo wa zamani wa Marekani.    

Kevin Rojek (katikati) Afisa Maalum anayesimamia Ofisi ya FBI huko PittsburghPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Shirika la upelelezi la Marekani la FBI limesema mwanamume huyo aliyeuwawa mara tu baada ya kufanya  shambulio hilo, ametambuliwa kuwa ni kijana Thomas Matthew Crooks mwenye miaka 20 na mkaazi wa jimbo la Pennsylvania. Uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema walimuona mtu mwenye silaha kabla ya shambulio hilo na waliziarifu mamlaka. Hata hivyo polisi wamesema walipokea taarifa kadhaa za shughuli zenye kutia shaka, bila kufafanua zaidi. Mtu mmoja aliyekuwa katika mkutano huo aliuwawa huku mwengine akijeruhiwa vibaya.

Timu ya  kampeni ya Trump  imeongeza idadi ya maafisa wenye silaha katika maeneo ya kampeni kufutatia tukio hilo. Wafanyakazi wa kikosi cha kampeni cha Trump huko Washington na West Palm wametakiwa siku ya Jumapili kutowasili kwenye ofisi zao kutokana na sababu za kiusalama.

Donald Trump amesema siku ya Jumapili kuwa anatarajia kuzungumza huko Wisconsin kunakotarajiwa wiki hii Kongamano la Kitaifa la chama cha Republican. Hata hivyo wanasiasa na wafuasi wa Trump wameshauriwa kutotoa maoni yao juu ya tukio hilo, wakati huu uchunguzi ukiendelea.

(Vyanzo: Mashirika)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW