1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi na wadau wa Bundesliga kujadili hatima ya msimu huu

Sekione Kitojo
16 Machi 2020

Viongozi na  wadau wa  Bundesliga  wakutana  kuamua  hatima  ya msimu  huu  wa  ligi. Michezo ya Bundesliga hivi sasa imesitishwa kutokana na kitisho cha virusi vya Corona.

Viongozi  wa  Bundesliga walikuwa wanatafakari  kufanya maamuzi makali  kabla  ya  mkutano  wao  leo  mjini  Frnkfurt ambao unatarajiwa  kuthibitisha  kusitishwa  kwa  michezo hadi  mapema mwezi  ujao.  Rais  wa  heshima  wa  Bayern Munich Uli Hoeness amesema  "Hakuna  muongozo maalum" wa  namna  gani  ya kufanya  kupambana  na  dharura  hii  ya  kuzuka  kwa   virusi  vya Corona na  kutoa  wito  kwa  wapenzi  wa  kandanda  kuwa wavumilivu.

Rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani Fritz KellerPicha: Imago Images/J. Huebner

Hatimaye  tunapaswa  kukubali  hali  halisi. Inatubidi  kusubiri  kwa wiki  nne, na  kuanza  upya kabisa.  Huenda  tunapaswa  kusitisha kucheza  kandanda  mwezi  Oktoba,"  amesema  katika  televisheni ya  Sport 1. Wadau wa  ligi  wanatarajiwa  kujadili  hali  mbali  mbali ikiwa  ni  pamoja  na  uwezekano wa  msimu  kufutwa  kabisa. Lakini Fernando Carro mtendaji mkuu  wa  Bayer Leverkusen ameliambia shirika  la  habari  la  DPA: "kufutwa kwa  mashindano  yote  kwa sababu  nyingi sio jambo linalofikiriwa."

Mashabiki wa kandanda nchini Ujerumani wakipinga kuchezwa michuano ya ligi bila mashabikiPicha: picture-alliance/dpa/J. Güttler

Kamati ya  kimataifa  ya  Olimpiki IOC, itafanya  mazungumzo na wakuu  wa  mashirika  la  kimataifa  ya  michezo  kesho Jumanne katika  juhudi  za  kuchukua  hatua  dhidi  ya  kuzuka  kwa  virusi  vya Corona, duru  karibu  na  shirikisho  hilo  la  kimataifa  limesema katika  taarifa  yake.

Ikiwa  chini  ya  miezi  mitano  hadi  kuanza kwa  mashindano  ya  Olimpiki   mwaka  2020  mjini  Tokyo  hapo Julai 24, maswali  yamezuka  kuhusiana  na  iwapo  michezo  hiyo kwamba  inaweza  kufanyika ama  la. Wakati  huo  huo  michuano ya kufuzu kucheza  katika  michezo  hiyo  ya  olimpiki  kwa  wana masumbwi kutoka  barani  Ulaya  itafanyika  mjini  London leo bila mashabiki licha  ya  wasi  wasi  unaoongezeka  kuhusiana  na  virusi vya  Corona na  kuparaganyika  kwa  kiasi  kikubwa  kwa  matukio ya  michezo  duaniani  kote.

Rais wa heshima wa Bayern Munich Uli HoenessPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schrader

Virusi  ambavyo  vimeanzia  huko  nchini  China  mwishoni  mwa mwaka  jana, vimewauwa  zaidi ya  watu 6,000 duniani  kote  na kuwaambukiza  zaidi  ya  watu 160,000.

Kuzuka  kwa  virusi  hivyo  kumeleta  mtafaruku  katika  kalenda  ya michezo  duniani , na  kusababisha  kufutwa  kwa michuano  ya kufuzu  kucheza  katika  michezo  hiyo  ya  Olimpiki na  wasi  wasi umeongezeka  juu  ya  iwapo michezo  yote inapaswa  kufutwa  ama kuahirishwa.

Hali  ya  shaka shaka  inaongezeka  nchini  Japan juu  ya  michezo hiyo  ya  Olimpiki, kukiwa  na  upinzani  mkubwa  wa  kutaka kuendelea   na  michezo  hiyo  kama  ilivyopangwa  na  wengine wakiwataka  maafisa  kutohatarisha  maisha  kwa  kulazimisha kuendelea  na michezo  hiyo  katika  wakati  huu  wa  dharura  ya virusi  vya  Corona.

Rais wa IOC Thomas BachPicha: picture-alliance/TT NYHETSBYRÅN/S. Stjernkvist

Maafisa  kama  waziri  mkuu  wa  Japan  Shinzo  Abe  na  mkuu  wa kamati  ya  kimataifa  ya  Olimpiki Thomas Bach wamekwisha sisitiza  mara  kadhaa  kwamba  matayarisho  yaendelee  kuwasha mwenge  wa  olimpiki  hapo Julai 24.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW