1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiTanzania

Viongozi Tanzania wadai kutishiwa kuhusu suala la Bandari

Florence Majani12 Julai 2023

Suala la uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World Dubai bado linaendelea kugonga vichwa vya habari nchini Tanzania. Hii ni baada ya viongozi kadhaa kudai kutishiwa kuuawa

AfCFTA
Bandari ya Dar es Salaam inachangia pakubwa katika uchumi wa TanzaniaPicha: Xinhua News Agency/picture alliance

Aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden na kabla ya hapo katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa, mawakili na mwakilishi wa viongozi wa dini, wameibuka na madai ya kutishiwa kuuawa kwa kile wanachosema ni kuwa na msimamo wa kupinga Mkataba wa Uwekezaji wa Bandari kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.

Soma pia: CCM yabariki uwekezaji bandari nchini Tanzania

Akiambatana na mawakili Peter Madeleka na Boniface Mwabukusi, Balozi huyo wa zamani wa Tanzania nchini Sweden ameitisha mkutano wa waandishi wa habari kuezungumzia mkataba wa bandari kati ya serikali ya Tanzania  na kampuni ya DP World, na kudai  kuwa wametishiwa kuuawa kutokana na misimamo yao ya kuukosoa mkataba huo.

Kwa upande wake, Dk. Slaa, aliyewahi kuvuma miaka ya 2000 kutokana na kuwa kinara wa upinzani kabla ya kuachana na chama chake na kuteuliwa na Marehemu Rais John Magufuli  kuwa balozi, amesema mbali ya vitisho kwa maisha yake, ametishiwa kunyang'anywa hata hadhi yake ya ubalozi.

Balozi Slaa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameliingiza taifa kwenye msiba kwa kujua au kwa kutokujua kwani alitakiwa atafute washauri kabla ya kuingia katika mktaba huo.

Kwa upande wake, Wakili Boniface Mwabukusi amesema yeye pamoja na wenzake wamekuwa wakitolewa vitisho na wito wa kuitwa na jeshi la polisi kutokana na msimamo wao katika kukosoa mkataba huo wa bandari, lakini akaapa kuwa kamwe  hawatatetereshwa na vitisho hivyo.

Soma pia: Maandamano ya kupinga uwekezaji wa Dubai katika bandari ya Tanzania yazimwa

Huku wakionyesha nakala ya wito wa kuitwa na jeshi la polisi, mawakili hao pamoja na Dk Slaa wamerejea msimamo wao kuwa serikali imekiuka kanuni na sheria na kwamba mkataba huo haufai kwa mustakabali mwema wa Watanzania. Wakili Peter Madeleka alikuwa na haya ya kusema:

Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Ukonga kupitia chama tawala, CCM, na ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Miundombinu, Jerry Slaa, amesema Watanzania wanahitaji majibu baada ya kuwepo upotoshaji mkubwa kuhusu sakata la bandari:

Sakata linalohusisha uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam lilianza kushika kasi hivi karibuni baada ya kutangazwa mwekezaji huyo mpya, kampuni ya DP World kutoka Dubai, baada ya mwekezaji wa awali kumaliza muda wake na kutokuongezewa muda na serikali inayodai kwa muda wa miongo mitatu muwekezaji huyo hakuwa ameifadisha nchi inavyostahiki.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW