1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika kujibu mapinduzi ya kijeshi Gabon

31 Agosti 2023

Viongozi wa Afrika wanashughulika kutafuta namna ya kujibu hatua iliyochukuliwa na maafisa wa kijeshi nchini Gabon ya kumuondowa madarakani rais Ali Bongo na kumuweka kiongozi wao madarakani.

ECOWAS Meeting
Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi,ECOWAS jana alisema anashirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Afrika ,kudhibiti kile alichokiita utawala wa kimabavu unaosambaa barani Afrika.

Kwa mujibu shirika la habari la Reuters, msemaji wa tume ya Umoja wa Afrika,  amefahamisha kwamba baraza la amani na usalama la Umoja huo litakutana leo Alhamisi.

Soma pia:Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya wanaokutana nchini Uhispania wamesisitiza umuhimu wa demokrasia.

Taasisi mbali mbali za barani Afrika zimelaani mapinduzi ya Gabon ambayo kwa mujibu wa jeshi, yamechochewa na dosari kubwa za uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kanda ya Afrika ya Kati ECCAS pia imelaani mapinduzi hayo ikisema kupitia taarifa yake kwamba inapanga mkutano wa viongozi wakuu wa nchi kutazama hatua za kuchukuliwa.