Viongozi wa Afrika kutatua mzozo wa Ukraine
17 Mei 2023Rais Ramaphosa amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wameridhia kupokea ujumbe na wakuu wa nchi za Afrika mjini huko Moscow na Kyiv. Mwishoni mwa juma lililopita Ramaphosa alielezwa kufanya mazungumzo kwa njia ya simu kwa nyakati na Rais Putin na kadhalika Rais Zelensky, ambapo aliwasilisha jitihada iliyoandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Zambia, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Misri na taifa lake Afrika Kusini.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Cape Town, wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Hsien Loong. Ramaphosa amesema amekubaliana na pande hizo hasimu kuanza maandalizi ya mazungumzo na viongozi wa Afrika na kwamba anatarajia kufanyika makubaliano ya kina. "Majadiliano yangu na viongozi hao wawili yalionyesha kuwa wote wako tayari kupokea viongozi wa Afrika na kuwa na majadiliano juu ya jinsi mzozo huu unaweza kumalizwa. Ikiwa hilo litafaulu au la itategemea majadiliano yatakayofanywa,"alisema Ramaphosa
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika unataarifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Umoja wa Afrika wamepewa taarifa kuhusu mpango huo. Hata Ramaphosa hakutoa ratiba maalum ya ziara hiyo au maelezo mengine ya ziada , lakini amesema tu kwamba mzozo wa Urusi na Ukraine umekuwa wa kuangamiza na Afrika pia inateseka sana kutokana na vita hiyo.
Nchi za Afrika zimeathiriwa vibaya na kupanda kwa bei ya nafaka na athari kwa biashara ya dunia. Tangazo limetolewa siku moja baada ya Ramaphosa kusema Afrika Kusini imekuwa katika shikikiza kubwa la kuchagua upande katika mzozo huo, kufuatia shutuma kutoka kwa Marekani kwamba Pretoria inaipa silaha kwa serikali ya Moscow hatua ambayo ingevunja ahadi yake kutoegemea upande wowote.
Majeshi ya Ukraine yawafarushwa wa Urusi kandoni mwa Bakhmut
Ndani nchini Ukraine, Serikali ya taifa hilo imesema imefanikiwa kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi kutoka pembezoni mwa mji unaogombaniwa wa Bakhmut lakini pia imekiri kwamba vikosi vya Moscow vilikuwa vinaingia ndani zaidi ndani ya mji huo uliovurugwa kwa vita.
Soma zaidi:Urusi: Ukraine imetumia makombora ya Uingereza kuwalenga raia
Tangazo hilo limetolewa wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema viongozi wa Ulaya wanaokutana nchini Iceland wamekikubaliana kuunda kile walichokiita "orodha la uharibifu" ili kurekodi madhara na uharibifu wa wakati wa vita uliofanywa na Urusi nchini Ukraine. Mwaka mmoja baada ya kuiondoa Urusi katika Baraza la Ulaya (CoE) kutokana na vita vyake nchini Ukraine, viongozi wa baraza hilo lenye mataifa 46 wanakutana mjini Reykjavik, ajenda kuu ikiwa mzozo wa Ukraine.
Chanzo: AFP
Mhariri: Daniel Gakuba