1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika wahimiza matumizi ya nishati jadidifu

Thelma Mwadzaya6 Septemba 2023

Viongozi wa Afrika wametaka mabadiliko makubwa katika mfumo wa fedha wa kimataifa na kuihimiza jumuiya ya kimataifa kuunga mkono ongezeko la nishati jadidifu.

Ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Kenyatta International Convention Centre (KICC) Nairobi
Viongozi waliohudhuria mkutano wa kilele wa mazingira jijini NairobiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Rais wa Kenya William Ruto ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kilele wa siku tatu, amesema viongozi wameidhinisha Tangazo linaloangazia uwezo wa bara la Afrika kama nguvu kuu katika suala la ulinzi wa mazingira.

Akihitimisha Kongamano hilo la Kilele la kwanza barani Afrika kuhusu masuala ya tabia nchi, Rais William Ruto alishikilia kuwa suluhu zinazopendekezwa na Afrika ni za manufaa kwa ulimwengu mzima.

Viongozi wa Afrika wanaitolea wito jamii ya kimataifa kulipa uzito suala la tabia ya nchi kwa kupunguza viwango vya Gesi za viwandani, kusaka njia za kuhimili athari zake, kufadhili miradi endelevu na kutimiza ahadi za awali ilizopewa Afrika. 

Kwenye majadiliano hayo ya siku tatu, Afrika imepokea ahadi za dola bilioni 23 za kufadhili miradi ya kulinda mazingira na mbinu mujarab za kuhimili madhila ya tabia ya nchi.

Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Sierra Leone Julius Maada Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Wakuu wa nchi na serikali za Afrika wamependekeza kuundwa mpango maalum wa fedha utakaotilia maanani utaratibu tofauti wa kulipa madeni kadhalika kuzipa serikali afueni. Viongozi hao wameafikiana kuandaa mpango mpya kupitia baraza kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kongamano la washirika kuhusu masuala ya tabia ya nchi ifikapo mwaka 2025. 

Afrika yaathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

This browser does not support the audio element.

Wakati huohuo, wabunge wa Afrika wanatiwa shime kukumbatia uzalendo wanapokabiliana na masuala ya tabia nchi. Haya yamejiri kwenye mjadala wa wabunge uliowaleta pamoja viongozi 500 wa mataifa mbalimbali barani Afrika waliokutana kwenye Majengo ya bunge la Taifa.

Akilihutubia bunge, Spika wa Taifa Moses Wetangula aliusisitizia umuhimu wa bara la Afrika kuchukua nafasi yake katika Ajenda ya kupambana na madhara ya tabia nchi Ijapokuwa sio mchafuzi mkubwa wa mazingira na aghalabu linatengwa kwenye jukwaa la kimataifa.

Ruto asema mabadiliko ya tabianchi yanatafuna maendeleo ya Afrika

Suala lililohanikiza ni Afrika kuwezeshwa kuvumbua mbinu mujarab za kuhimili makali ya tabia ya nchi. Wakfu wa Bezos umeahidi msaada wa dola milioni 22.8 kuhifadhi maeneo maalum yaliyo na uwezo wa kufyonza hewa ukaa ya Bonde la UFA nchini Kenya Pamoja na mabonde ya mito ya mto Rusizi na Ziwa Kivu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda na Burundi.

Ifahamike kuwa wiki ya masuala ya tabia nchi inaendelea hadi tarehe 8 mwezi huu. Maazimio ya leo yatawasilishwa kwenye kikao kijacho cha mazingira COP 28kitakachofanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwaka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW