Viongozi wa Afrika wahutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
22 Septemba 2023Viongozi hao kadhaa wa Afrika waliohutubia kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni pamoja na rais wa Kenya William Ruto na rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Toudera ambaye amezilaumu nchi za magharibi kwa kusababisha mgogoro wa wakimbizi kutokana na kupora raslimali za nchi za Afrika.
Rais Touadera amezungumzia juu ya maalfu ya wakimbizi wa Afrika waliowasili, kwenye kisiwa cha Italia cha Lampedusa wiki iliyopita. Amesema vijana wanaoondoka Afrika na kwenda Ulaya ndio wanaopaswa kuwakilisha Afrika ya leo na mustakabal wake lakini ameeleza kuwa vijana hao wanakimbilia Ulaya ili kutafuta maisha bora na ameeleza kwa nini, amesema mgogoro wa wakimbizi ni miongoni mwa matokeo ya kuporwa kwa raslimali za nchi ambazo zimefanywa kuwa masikini kutokana na utumwa na ukoloni na ubeberu wa nchi za magharibi.
Soma:Ujerumani, Brazil, Japan na India zataka mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Rais huyo wa Jamhuri ya Afrika ya kati Touadera amesifu mshikamano na juhudi za pamoja zinazofanywa na nchi zinazowahifadhi wakimbizi lakini ameshauri haja ya kuzipa nchi za Afrika sauti kubwa zaidi kuhusu kuutatua mgogoro wa wakimbizi. Rais Toudera ameutaka Umoja wa Mataifa uzihusishe zaidi nchi za Afrika katika juhudi za kutafuta suluhisho la migogoro ya dunia.
Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mkuu wa majeshi ya Sudan jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametahadharisha kwamba vita vya nchini mwake vinaweza kuenea kwenye eneo lote la nchi zinazopakana na Sudan. Jenerali Burhan ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba vita hivyo kati ya pande mbili hasimu za jeshi ni kama cheche inayoweza kuwasha moto kwenye ukanda wa nchi zinazopakana na Sudan.
Rais wa Kenya William Ruto, akichangia kwenye mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuwekeza katika sekta za tekinolojia, miundo mbinu na kilimo ili kuwawezesha vijana wa Afrika kumudu maisha yao nyumbani na hivyo kuzuia mawimbi ya wakimbizi kutoka bara hilo.
Naye kiongozi wa kijeshi wa Guinea, Mamady Doumbouya amesema demokrasia ya nchi za magharibi haiwezi kuleta tija barani Afrika kama jinsi ilivyoshuhudiwa katika mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Niger, Burkina Faso, Chad,Gabon na Mali.
Soma:Viongozi wahutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Kwa upande wake rais wa Nigeria Bola Tinubu ameutaka Umoja wa Mataifa kuwa makini katika masuala ya umaskini na usalama barani Afrika na pia ametaka nchi yake isaidiwe kupambana na uchimbaji haramu wa rasilimali za nchi yake.
Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas pia alihutubia kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Amesema kwamba mashariki ya kati haiwezi kuwa na amani bila ya haki za wapalestina kuzingatiwa. Mahmoud Abbas amesema wale wanaofikiria kwamba amani inaweza kudumu katika mashariki ya kati bila ya haki kamili za kitaifa za wapalestina, wanafanya makosa.
Viongozi wengine wanatarajiwa kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalofanyika kwa mara ya 78 mnamo mwaka huu.
Vyanzo:AFP/RTRE/DW