Viongozi wa Afrika waijadili Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo
5 Novemba 2013Kauli hiyo ya viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imesadifiana na tangazo la waasi hao kuwa wako tayari kumaliza uasi wao uliodumu kwa muda wa miezi 20 katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika tangazo lao la leo, waasi hao wamesema wako tayari kuweka silaha chini na kushiriki kwenye utaratibu wa kuupatia mzozo huo suluhisho la kisiasa. Tangazo hili la M23 limekuja masaa kadhaa baada ya wanajeshi wa serikali kuwang'oa waasi hao kutoka ngome zao mbili za mwisho majira ya 9 alfajiri ya leo, kwa saa za Afrika ya Kati.
Katika mkutano huo wa SADC kulijadiliwa kuwa masuala 11 yaliyoko katika mazungumzo ya Kampala yamekubaliwa na kwamba pande husika zitatia saini makubaliano hayo kwa sharti tu iwapo M23 itatangaza hadharani kuwa imeachana na uasi.
Hayo ni kulingana na Katibu Mtendaji wa SADC, Stergomena Tax. M23 iliingia katika mazungumzo ya kutafuta amani ya Kongo na serikali yanayofanyika mjini Kampala, Uganda, lakini mazungumzo hayo yalisambaratika mwezi uliopita na kusababisha jeshi la Kongo kufanya mashambulizi dhidi ya waasi hao.
Jeshi la Congo lasifiwa
Mkutano huo unaofanyika mjini Pretoria, Afrika ya Kusini pia umelisifu jeshi la Kongo kwa ushirikiano na Kikosi Maalum cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) kwa kuwafurusha waasi wa M23 kutoka ngome zao na kurejesha udhibiti.
Kikosi cha MONUSCO chenye wanajeshi 3,000 kinawajumuisha wanajeshi kutoka Malawi, Afrika ya Kusini na Tanzania na kina jukumu la kukabiliana na waasi mashariki mwa Kongo. Kinajiunga na walinda amani 17,000 ambao tayari wako sehemu mbali mbali nchini humo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini alisema hatua muhimu zinachukuliwa na zinasisitizwa na mchakato wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta amani na usalama nchini Kongo na kanda ya Maziwa Makuu ili kufikia suluhisho la kisiasa na kubaini vyanzo vya kimsingi vya mzozo katika kanda hiyo.
Marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Uganda na Zimbabwe walikuwa miongoni mwa viongozi wa nchi waliohudhuria mkutano huo wa Pretoria.
Mwanzo mpya kwa Congo baada M23 kufurushwa
Kamishna wa Umoja wa Afrika kuhusu amani na usalama, Smail Chergui, alisema mkutano huo unajaribu kuandika ukurasa mpya wa historia wa kanda hiyo iliyokumbwa na majanga.
Mwenyekiti wa SADC na ambaye pia ni Rais wa Malawi, Joyce Banda, ameitaka serikali ya kongo kuzingatia kurejea katika meza ya mazungumzo na waasi kwa kile alichokiita kwa ajili ya amani ya Kongo, kwani hatua za kijeshi pekee haziwezi kuutatua mzozo huo.
Rais Paul Kagame wa Rwanda hakuhudhuria mkutano huo wa jana lakini Rais Yoweri Museveni wa Uganda alikuweko na alisema kuzuka upya kwa mapigano nchini Kongo hakukutarajiwa. Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwasaidia waasi nchini Kongo madai ambayo nchi hizo imeyakanusha.
Leo Afrika ya Kusini inakuwa mwenyeji wa mkutano mwingine utakaozungumzia kuundwa kwa kikosi cha kijeshi cha Afrika kitakachokuwa kikitumwa popote penye mizozo barani humo.
Mwandishi: Caro Robi/Afp
Mhariri: Mohammed Khelef