Viongozi wa Afrika wataka mataifa yaliondelea yawajibike
2 Desemba 2023Viongozi wa mataifa yanayoendelea Jumamosi hii wameingia katika siku yao ya pili ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa shinikizo kwa mataifa tajiri yalioendelea kiviwanda kutoa ujuzi wao wa namna ya kukabiliana na ongezeko la joto duniani, kadhalika kupunguza mzigo wa ukataji fedha unaowakabili.
Viongozi hao wameyasema hayo huku wakipigia chapuo maliasili zao wenyewe ambazo zinasaidia katika kupungua hewa ya kaboni inayoongeza joto.
Viongozi wa Afrika walibainisha kuwa misitu ya mvua ya bara lao inasaidia kupunguza kiwango cha kaboni ya ziada angani, na mataifa yao yanachangia kiwango kidogo katika uzalishaji wa hewa hiyo ikilinganishwa na mataifa tajiri.
Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema amesema mataifa yaliondelea yameshindwa kutekeleza ahadi zao za kuchangia fedha katika makabiliano ya ustawi wa hali ya hewa na kufikia malengo yao wenyewe katika kudhibiti uchafuzi unaofanywa na viwanda vyao.
Mkutano wa kila mwaka wa wanachama wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama COP28, katika Umoja wa Falme za Kiarabu zenye utajiri mkubwa wa mafuta unashirikisha marais wapatao 150, mawaziri wakuu, wafalme na viongozi wengine kwa shabaha ya kupunguza kitisho cha ongezeko la joto duniani.