1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa chama cha kijani Ujerumani waachia ngazi

25 Septemba 2024

Viongozi wa Chama cha Kijani kilichomo kweye serikali ya muungano nchini Ujerumani inayoongozwa na kansela Olaf Scholz, wametangaza kujiuzulu nyadhfa zao kwenye chama hicho.

Viongozi wa Chama cha Kijani Ricarda Lang na Omid Nouripour
Viongozi wa Chama cha Kijani Ricarda Lang na Omid Nouripour Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Viongozi hao Ricarda Lang na Omid Nouripour, walitangaza siku ya Jumatano kuwa watendaji wakuu wote wa chama cha Kijani cha walinda mazingira watajiuzulu ifikapo mwezi Novemba baada ya chama hicho kushindwa vibaya kwenye chaguzi kadhaa za mikoa.

Mmoja wa viongozi hao Omid Nouripour, ameeleza kwamba chama hicho cha walinda mazingira kinakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi katika kipindi cha muongo mmoja baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi kwenye majimbo ya mashariki zilizofanyika mwezi huu.

"Tumeamua katika Kamati ya Kitaifa ya Utendaji kuwa ni wakati sasa wa kukikabidhi chama hiki kikubwa katika mikono mipya na hivyo tunawaomba wana Mazingira wa chama chetu cha Kijani tunachokipenda kwamba katika mkutano ujao wa chama utakaofanyika katika mji wa Wiesbaden, wachague uongozi mpya."

Kiongozi mwenzake Ricarda Lang amesema baada ya cha hicho kupata matokeo mabaya katika chaguzi kwenye majimbo matatu uongozi wa chama cha Kijani umekuwa ukikabiliwa na shinikizo la kujiuzulu na sasa viongozi hao baada ya kutafakari wamechukua uamuzi huo.

"Sura mpya zinahitajika kukiongoza chama na kukiondoa kwenye mgogoro huu unaotukabili. Kama mjuavyo huu si uamuzi rahisi kuufanya, lakini tuna Imani kubwa tunapoutangaza uamuzi huu. Inawezekana kuwa ni msingi wa kujenga upya mkakati wa chama hiki. Na hiki ndicho kinahitajika.”

Kiongozi wa chama cha kijani Omid NouripourPicha: Frank Hammerschmidt/dpa/picture alliance

Nouripour na kiongozi mwenzake, Ricarda Lang, walichukua nafasi hiyo ya uongozi wa chama cha Kijanimapema mwaka 2022 baada ya viongozi watangulizi Robert Habeck na Annalena Baerbock walipojiunga na serikali ya Kansela Olaf Scholz kama makamu wa Kansela na waziri wa mambo ya nje.

Chama cha Kijani ni cha pili kwa ukubwa katika serikali ya muungano wa vyama vitatu ya Ujerumani pamoja na chama cha mrengo wa kati cha Social Democrats (SPD) kinachoongozwa na kansela Olaf Scholz na chama cha Waliberali cha Free Democrats (FDP).

Waziri wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock na Waziri wa Uchumi Robert Habeck ni wajumbe mashuhuri kwenye baraza la mawaziri la wanaotoka kwenye chama cha Kijani. Soma: Chama cha Kijani nchini Ujerumani chaonya udhibiti mipakani kuwa wa kudumu

Kutokana na kuwa Nouripour na Lang kuwa sio sehemu ya mawaziri wanaounda Baraza la Mawaziri la serikali ya kanseela Olaf Scholz, uamuzi wao wa kujiuzulu hautawaathiri mawaziri watano wa chama hicho cha Kijani waliomo kwenye Baraza la Mawaziri.

Mawaziri hao mabli na Robert Habeck waziri wa Uchumi na Ulinzi wa Hali ya Hewa na Annalena Baerbock waziri wa mambo ya nje, wengine ni Cem Özdemir Waziri wa kilimo, Steffin Lmke Waziri wa mazingira na Anne Spiegel Waziri anayehusika na maswala ya familia.

Viongozi wa Chama cha kijaniPicha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Soma: Mkwamo wa bajeti watishia kuivunja serikali ya Ujerumani

Miongoni mwa matukio mabaya ya hivi karibuni kwa chama hicho cha Kijani ni uchaguzi uliomalizika wa siku ya Jumapili katika jimbo la mashariki mwa Ujerumani la Brandenburg, ambapo chama hicho kilipoteza viti vyote katika bunge kwenye jimbo hilo baada ya kushindwa kufikia kiwango cha asilimia 5 kinachohitajika ili kupata uwakilishi bungeni katika uchaguzi wa Ujerumani.

Serikali ya sasa imeshuhudia umaarufu wake ukishuka huku kukiwa na mabishano ya ndani na uchumi uliokwama.

Vyama vyote vitatu vilipata misukosuko katika uchaguzi wa kikanda, huku chama cha FDP kikishindwa kuingia katika bunge lolote katika majimbo matatu ya Thruringia, Saxnoy na Brandenburg. Chama cha SPD chapata ushindi uchaguzi wa Brandenburg

Chama cha Kijani kilipata umaarufu kutokana na harakati zake za kupinga uharibifu wa mazingira, na kupinga matumizi ya nyuklia nchini Ujerumani mnamo miaka ya 70, na kimewahi kushiriki katika serikali za kitaifa zilizoongozwa na chama cha Social Democratic (SPD).

Vyanzo: DPA/AFP/AP/RTRE