1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dini Kenya wapewa kibarua cha kurejesha umoja

27 Januari 2023

Wakati viongozi wanaotawala Kenya wakipishana kwenye nyumba za ibada kushukuru kwa kuchaguliwa na wa upinzani wakiendelea kuhoji kuwa waliibiwa kura, viongozi wa dini wametakiwa kusimama imara kurejesha umoja wa kitaifa.

Kenia Nairobi | William Ruto gewinnt Präsidentschaftswahl
Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Akiongoza mkutano wa maombi ya shukrani uliowaleta pamoja viongozi wa kisiasa, mawaziri, viongozi wa kidini na maafisa wakuu wanaohudumu katika kaunti ya Nakuru, Gavana Susan Kihika aliwahimiza viongozi wa kidini kudhihirisha mchango wao kwa umma na kutoa mwongozo unaofaa.

Mchango wa kanisa kwenye siasa umesababisha mdahalo mkubwa nchini Kenya hasa baada ya kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja one Kenya, Raila Odinga, kumkosoa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana, Jackson Ole Sapit, kwa kuhusika kwenye siasa na kuegemea upande wa mpinzani wake, Rais William Ruto, wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga (katikati), bado anahoji uhalali wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Kwa upande wake, Askofu Sapit ametoa wito kwa wanasiasa kupunguza cheche zao na badala yake kuzingatia utangamano wa Wakenya na namna ya kuboresha hali ya uchumi wa Wakenya.

Mkuu huyo wa Kanisa la Anglikana nchini Kenya amekuwa akihimiza usawa baina ya viongozi walioko serikalini na wale walio kwenye upinzani.

Sikiliza zaidi: 

Kenya: Wito wa kuunda afisi ya kiongozi wa upinzani

This browser does not support the audio element.

"Ustawi wa taifa hili ni muhimu kwetu sote. Kenya inahitaji kuimarika kwa kuboresha mahusiano kati yetu, tuvunje misingi ya kikabila na kusonga mbele pamoja. Tunahitaji pia kuimarika kiuchumi, kwa kuangazia mambo yanayowaathiri wakenya kama vile gharama ya juu ya maisha. Lakini tutaweza kufikia haya iwapo kutakuwa na mazingira mazuri ya kisiasa." Alisema Askofu Sapit.

'Kesi mahakamani zakwamisha maendeleo'

Gavana Kihika, ambaye alifunguliwa kesi mahakamani alipoanza tu mchakato wa kuunda serikali yake baada ya kutwaa ushindi kwenye uchaguzi wa Agosti, alisema kesi za mara kwa mara mahakamani zinakwamisha utoaji wa huduma kwa umma.

Rais William Ruto akiapishwa kushika madaraka yake tarehe 13 Septemba 2022.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Gavana huyo alitumia hafla hiyo kutangaza kuanzishwa kwa miradi mbalimbali, ikiwemo kufufuliwa kwa mradi wa Bwawa la Itare unaofanywa kwa ushirikiano na Italia.

Soma zaidi: Ruto atoa amri ya mabadiliko ya utendakazi wa wizara Kenya

Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza mkutano wa maombi ya shukrani utakaofanyika mjini Nakuru tarehe 12 mwezi ujao.

Mkutano huo utawaleta pamoja viongozi na Wakenya wa tabaka mbalimbali kutoka kote nchini.

Mji wa Nakuru ni eneo muhimu kwa siasa za taifa la Kenya, kutokana na kwamba una wananchi wa makabila mbalimbali na pia mingi ya mikataba ya kisiasa iliyotengeneza serikali imefanyika huko.

Imeandikwa na Wakio Mbogho, DW Nakuru