1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kongo na Rwanda kufanya mazungumzo nchini Angola

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
5 Julai 2022

Angola ambayo ni mpatanishi kati ya Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema, marais wa nchi hizo mbili wanatarajiwa kukutana kwa mazungumzo mjini Luanda mnamo wiki hii.

Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame

Kulingana na taarifa kutoka kwenye ofisi ya rais wa Angola, mazungumzo kati ya Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame yanatarajiwa kufanyika hapo kesho Jumatano . Ofisi ya rais wa Angola pia imesema imefikia maelewano kwa viongozi hao wawili kukutana ana kwa ana katika mji mkuu wa pwani wa Angola, Luanda. Rais wa Angola Joao Lourenco, ambaye ni mpatanishi mkuu wa eneo la Maziwa Makuu, atakuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.

Rais wa Angola Joao LourencoPicha: Adrian Dennis/AFP/AP/picture alliance

Mkutano huo unafanyika wakati Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nchi kubwa yenye utajiri wa madini ikipambana kuyadhibiti makundi ya wapiganaji wenye silaha katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo, ambayo mengi ya makundi hayo yamekuwepo tangu kumalizika vita viwili vya kikanda katika muda wa robo karne iliyopita.

Kupamba moto kwa mapigano makali kumeufufua uhasama wa miongo kadhaa kati ya Kongo na Rwanda, huku Kongo ikiilaumu Rwanda kwa hatua ya kuibuka upya kwa harakati za kundi la wanamgambo wa M23. Rwanda imekanusha mara kwa mara kuwaunga mkono waasi hao na nchi zote mbili zikiendelea kulaumiana kwa mashambulizi yanayovuka mpaka. Kagame anailaumu Kongo kwa kuwaunga mkono waasi wanaoipinga serikali yake wa FDLR wenye makao yao nchini Kongo. Kundi hilo linatuhumiwa kuwajumuisha wapiganaji walioshiriki katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mnamo mwaka 1994.

Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Estácio Valoi/DW

Viongozi wa Afrika Mashariki walikubaliana katika mkutano uliofanyika mwezi uliopita nchini Kenya kupeleka kikosi cha pamoja ili kusaidia katika kuzimaliza ghasia mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema hana tatizo kwa wanajeshi wake kutengwa katika kikosi hicho cha kikanda kilichopendekezwa kwa ajili ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais wa Angola Joao Lourenco mnamo mwezi Mei alifanikisha makubaliano yaliyowezesha kuachiwa wanajeshi wawili wa Rwanda waliokuwa wamekamatwa katika ardhi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bintou Keita, wiki iliyopita alitahadharisha kwamba mapigano yanaweza kuenea na kuwa mabaya zaidi na amezitaka pande zinazohusika kuchukua jitihada ya kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.

Vyanzo:AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW