Viongozi wa DRC hawataki wasimamizi wa Uchaguzi
24 Agosti 2018Umoja wa Mataifa, Afrika Kusini, Umoja wa ulaya na wengineo, wote hao jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, inasema haihitaji msaada wao, washauri wao wala maoni yao kuhusu maandalizi ya uchaguzi uliopangawa kuitishwa Desemba 23 inayokuja.
Kinshasa inataka kuwaweka kando "wajumbe maalum" na wasimamizi wengineo, na zoezi la uchaguzi ambalo lengo lake kuu ni kupatikana kwa mara ya kwanza kipindi cha mpito kwa njia ya amani nchcini humo.
Hadi wakati huu ratiba inaheshimiwa tangu rais Joseph Kabila aliposema hatogombea tena na badala yake kumteuwa "mfuasi wake". Orodha ya muda ya wagombea inatarajiwa kutangazwa wakati wowote hii leo.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini pia hatakiwi
Jumatatu iliyopita viongozi wa mjini Kinshasa walipinga ripoti iliyotangazwa na vyombo vya habari, bila ya kuthibitishwa na serikali kuhusu kuteuliwa rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki kuwa "mjumbe maalum" katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.
"Nnaweza kukwambieni, hakutokuwepo tena na mjumbe maalum yeyote katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, hata kama ni Thabo Mbeki" alisema mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa rais Kabila, Barnabé Kikaya Bin Karubi.
Anawalaumu wajumbe hao na kudai wana mtindo wa kujigeuza "mabalozi wadogo", hawaheshimu mamlaka ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo."Tunataka kudhihirisha tuko huru", amesema kwa upande wake waziri wa mawasiliano Lambert Mende.
Viongozi wa Kinshasa wanataka kuficha ukweli wa mambo
Msimamo wa serikali ya Kinshasa dhidi ya wasimamizi wa Umoja wa mataifa, Umoja wa Ulaya na Afrika Kusini unaangaliwa kwa jicho la wasi wasi na wadadisi. Mtaalam wa masuala ya katiba kutoka mashirika ya kiraia André Mbata Mangu anasema tunanukuu" kuukataa ujumbe wa Thabo Mbeki ni dalili kwamba jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo inataka kuficha mambo mengi yasigunduliwe na jumuia ya kimataifa."
Siku chache kabla tume ya uchaguzi ilisema haihitaji ndege na helikopta za tume ya umoja wa Mataifa nchini Kongo-MONUSCO ili kusafirisha zana za uchaguzi katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba milioni mbili na laki nane na wapiga kura milioni 40 waliosajiliwa.
"Hatulazimishi" walijibu wakati ule maafisa wa tume ya Mosnuco."
Serikali ya mjini Kinshasa inapendelea kuwaona wanajeshi wa tume ya kulinda amani wa umoja wa mataifa-MONUSCO wakiihama nchi hiyo hadi ifikapo mwaka 2020.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga