1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia kuhutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa

24 Septemba 2024

Marais na viongozi wakuu wa mataifa wanaanza hivi leo kuhutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, huku ulimwengu ukikabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa, mgogoro wa Mashariki ya Kati na vita vya Urusi na Ukraine.

Mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.
Mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.Picha: Bianca Otero/ZUMA Wire/IMAGO

Mkutano huu wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa umepewa jina la 'hija ya wanadiplomasia' kwa kuwa kila mwaka hukusanyika kwenye eneo la mashariki mwa mji kitongoji cha Manhattan, kutoa ya nyoyoni mwao kwa yale yanayojiri kwenye mataifa yao, kanda zao na kwa ulimwengu kwa ujumla.

Mwaka huu, viongozi hao wanakutana katika wakati ambapo ulimwengu umekabiliwa na hali mbaya zaidi kuliko mwaka jana, ambapo mwenyeji wao, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliwaonya juu ya matatizo kadhaa yaliyokuwa yameilemea sayari ya dunia kwa wakati huo. 

Soma zaidi: Hotuba za viongozi UNGA kuuanza kutolewa rasmi Jumanne

Ifikapo majira ya saa 9:00 mchana kwa saa za New York, ambapo itakuwa sawa na 3:00 usiku hapa Ulaya ya Kati na 4:00 usiku Afrika Mashariki, Guterres anatazamiwa kuufunguwa mkutano wa mwaka huu kwa onyo lile lile la mwaka jana, na baada ya hapo viongozi wa dunia wataanza kupanda jukwaani mmoja baada ya mwengine.

Hotuba za migawanyiko ya dunia

Siku moja kabla ya mkutano huu, tayari kulishakuwa na ishara ya kile ambacho viongozi hao wangelikizungumzia, pale wengi wao walipopaza sauti zao kupitia Mkutano wa Kilele kwa Mustakabali, ambapo wengi walijikita kwenye vitisho vipya kwa dunia, yakiwemo mabadiliko ya tabianchi na vita vilivyozagaa kwenye nyanja za mapigano na kwenye mitandao na vifaa vya kieletroniki.

Mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.Picha: Selcuk Acar/Andalou/picture alliance

Gaza, Lebanon, Ukraine, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, zitakuwa sehemu muhimu kwenye hotuba za viongozi hao.

Soma zaidi: Mashambulizi ya Israel yauwa zaidi ya watu 270 Lebanon

Rais Masoud Peshkian wa Iran alizungumzia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Lebanon, ambapo vifaa vya kieletroniki vilitumika kama silaha, na mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh, mjini Tehran, akisema ulikuwa ushahidi wa mbinu za Israel kuivuta Iran kwenye vita vya moja kwa moja baina yao.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, aliliambia jukwaa hilo kwamba ulimwengu unahitaji sheria zenye mizania kwa ajili ya usalama na matumizi yanayofaa ya teknolojia ili kulinda mamlaka na haki za mataifa na sio kinyume chake.

Mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Wang Yi, alizungumzia mradi mashuhuri wa nchi yake, maarufu kama Belt and Road Initiative, BRI, ambapo kampuni za China zinajihusisha na ujenzi wa miundombinu na nishati, wakati huo huo akikosowa shutuma dhidi ya Beijing alizosema zinachochewa na washindani wake duniani. 

Soma zaidi: Hadhara kuu ya UN yaidhinisha mkataba wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa

Awali Guterres alikuwa ameonya kwamba changamoto za kimataifa zinasonga mbele kwa kasi zaidi kuliko uwezo wa chombo chake kuzitatuwa.

Kutokana na Umoja huo kushindwa kukomesha mauaji kwenye mizozo inayoendelea sasa ulimwenguni, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema Umoja wa Mataifa unaelekea kutokuwa na nafasi yoyote kwenye siasa wala usalama wa dunia.