1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Viongozi wa dunia waihimiza Israel kutolipiza kisasi

15 Aprili 2024

Viongozi wa dunia wanaishauri Israel kutolipiza kisasi baada ya Iran kufyetuwa mamia ya droni na makombora dhidi yake siku ya Jumamosi, ili kuepusha kanda hiyo kutumbukia kwenye mzozo zaidi.

Kansela wa Ujerumani Olaf SCholz
Kansela wa Ujerumani Olaf SCholzPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameitaka Israel kuchangia hatua zitakazotuliza mzozo katika kanda hiyo ya Mashariki ya Kati licha ya shambulizi la Iran dhidi yake. Kansela Scholz amewaambia waandishi wa habari mjini Shanghai, China kwamba vilevile Iran lazima ikomeshe uchokozi.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron amekiambia kituo cha Utangazaji cha BBC kwamba kwamba Uingereza haiungi mkono ulipizaji kisasi.

Baadhi ya serikali za Afrika nazo zimezihimiza Israel na Iran kuepusha kuchochea mgogoro zaidi.

Soma pia: Guterres: Mashariki ya Kati iko katika ukingo wa vita

Kwenye taarifa yake iliyochapishwa kwenye ukurasa wa X, Rais wa Kenya William Ruto amesema ingawa shambulizi la Iran dhidi ya israel linaashiria tishio kwa amani na usalama wa kimataifa, Israel inapaswa kujizuia zaidi katika jibu lake.

Wito kama huo pia umetolewa na serikali ya Afrika Kusini na Nigeria.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema nchi yake itafanya kila iwezalo kuepusha machafuko kuongezeka Mashariki ya kati, baada ya shambulizi la droni na makombora ambalo halikutarajiwa la Iran dhidi ya Israel. Amesema hayo alipozungumza na kituo cha utangazaji cha BFMTV.

Kulingana na Macron, watajaribu kuishawishi Israel kutojibu mashambulizi ya Iran kwa njia ya kuongeza uhasama.

Amesema lengo linapaswa, kushawishi mataifa katika kanda hiyo kuitizama Iran kama hatari au tishio, na kwamba wanapaswa kuongeza vikwazo na shinikizo dhidi ya shughuli za nyuklia ndani ya Iran.

Soma pia: Israel: Mashambulizi ya Iran hayatapoteza lengo letu Gaza

Macron amesema wanahitaji kusimama na Israel kuhakikisha wanailinda kikamilifu, lakini pia kuepusha mzozo kutanuka.

Ameongeza kuwa ndege za Ufaransa zilisaidia kudungua droni na makombora yaliyokiuka anga ya Jordan.

Katika tukio jingine, Ujerumani imemuita balozi wa Iran aliyeko Berlin kuhusiana na shambulizi la Iran dhidi ya Israel.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema hayo na kuongeza kuwa tayari wanafanya mazungumzo.

Kulingana na msemaji huyo, Iran ilimuita balozi wa Ujerumani mjini Tehran jana Jumapili kuhusiana na kile ilichokiita kuwa misimamo isiyowajibika ya Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ambao pia mabalozi wao waliitwa.

SOma pia: Biden amrai Netanyahu dhamira ya kulipa kisasi dhidi ya Iran

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, taifa hilo lilifanya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya adui yake mkuu Israel kwa kurusha ndege zisizo na rubani 300 na makombora kadhaa.

Israel na washirika wake waliweza kuzuia takriban makombora na droni zote.Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Lakini Israel na washirika wake waliweza kuzuia takriban makombora na droni zote.

Iran ilisema shambulizi hilo lilikuwa ulipizaji kisasi kufuatia tukio la kuuawa kwa afisa wake wa ngazi ya juu wa jeshi kwenye shambulizi lililofanywa katika ubalozi wake nchini Syria.

Hayo yakitokota, kwingineko, wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon wamedai kulipua mabomu kuwalenga wanajeshi wa Israel, ambao wamedai walivuka na kuingia ndani ya Lebnon.

Jeshi la Israel lilisema wanajeshi wake wanne walijeruhiwa usiku wa kuamkia leo kwenye mlipuko katika eneo la mpaka wao wa kaskazini, lakini bila ya kueleza kundi lililohusika na shambulizi hilo.

Vyanzo: AFPE, DPAE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW