1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAustralia

Ulimwengu waungana kulaani shambulio la kigaidi Bondi Beach

Iddi Ssessanga afpe, rtre, ape
14 Desemba 2025

Viongozi wa dunia, mashirika ya kimataifa na jumuiya za kidini wamelaani shambulio la risasi lililoua watu 11 katika ufukwe wa Bondi Beach, Sydney, wakilieleza kuwa kitendo cha kigaidi chenye chuki dhidi ya Wayahudi.

Australia, Sydney 2025 | Shambulio la risasi Bondi Beach | Wahudumu wa uokoaji wakiwasafirisha majeruhi
Wahudumu wa dharura wakimsafirisha mtu kwenye machela baada ya shambulio la risasi lililoripotiwa katika ufukwe wa Bondi Beach mjini Sydney, Jumapili, tarehe 14 Desemba 2025.Picha: Mark Baker/AP Photo/picture alliance

Shambulio la risasi lililotokea Jumapili katika ufukwe maarufu wa Bondi Beach mjini Sydney limezua mshtuko na hasira duniani kote. Watu wasiopungua 12 waliuawa katika tukio hilo lililotokea wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah.

Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, alilitaja shambulio hilo kuwa la kushtua na la kuhuzunisha. Alisema ni tukio lisiloelezeka na lililotangazwa rasmi na polisi kuwa shambulio la kigaidi.

Rais wa Israel, Isaac Herzog, alilaani tukio hilo akisema ni shambulio katili dhidi ya Wayahudi. Aliwataja wahusika kama magaidi waovu waliolenga raia wasio na hatia.

Mfalme Charles wa Tatu, mkuu wa Jumuiya ya Madola, alisema ameshtushwa na kile alichokiita shambulio baya zaidi la kigaidi lenye chuki dhidi ya Wayahudi. Alitoa pole kwa waathiriwa na familia zao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema chuki dhidi ya Wayahudi haina nafasi duniani. Alisema mawazo na maombi ya Wamarekani yako pamoja na waathiriwa na watu wa Australia.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema ameshtushwa na kitendo hicho cha vurugu. Alisisitiza kuwa Ulaya inasimama pamoja na Australia na jamii za Kiyahudi kote duniani.

Mandhari ya angani inaonyesha wahudumu wa dharura wakifanya kazi katika eneo la tukio la shambulio la risasi katika ufukwe wa Bondi Beach mjini Sydney, Australia, tarehe 14 Desemba 2025.Picha: Nine Network/Seven Network/Australian Broadcasting Corporation/Handout via REUTERS

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alisema alipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za shambulio hilo. Alitoa rambirambi kwa familia za waathiriwa na jamii yote iliyoathiriwa.

Ugaidi na mauaji ya binadamu havikubaliki popote

Iran, ambayo ni adui mkubwa wa Israel, pia ililaani shambulio hilo. Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema ugaidi na mauaji ya binadamu hayakubaliki popote pale.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema Ufaransa itaendelea kupambana bila kuchoka dhidi ya chuki ya Kiyahudi. Alieleza mshikamano wake na waathiriwa wa shambulio hilo.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alisema alipokea kwa huzuni kubwa taarifa za vifo vya Sydney. Alisisitiza kuwa Italia inalaani aina zote za vurugu na chuki dhidi ya Wayahudi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, alisema ameshtushwa sana na shambulio hilo. Alilitaja kama kitendo cha chuki kilicholenga Wayahudi duniani kote siku ya kwanza ya Hanukkah.

Polisi wenye silaha wakifanya kazi katika eneo la tukio baada ya shambulio la risasi katika ufukwe wa Bondi Beach mjini Sydney tarehe 14 Desemba 2025.Picha: David Gray/AFP

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alisema nchi yake inasimama bega kwa bega na Australia. Alisisitiza kuwa ugaidi na chuki lazima zishindwe kila mahali.

Nchini Australia, Baraza la Kitaifa la Maimamu pia lililaani shambulio hilo. Lilitoa wito kwa Waaustralia wote kusimama pamoja kwa umoja na mshikamano.

Baraza hilo la Kiislamu liliwataka raia kuonyesha huruma kwa waathiriwa na familia zao. Lilisema vurugu hizo zimeacha majeraha makubwa ya kisaikolojia.

Kwa upande mwingine, mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi Australia, Robert Gregory, alisema shambulio hilo lilikuwa janga lililotarajiwa.

Alidai serikali ilikuwa imeonywa mara kadhaa lakini haikuchukua hatua za kutosha kulinda jamii ya Wayahudi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW