Viongozi wa dunia walaani shambulio la bunduki Urusi
23 Machi 2024Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake Farhan Haq amelaani shambulio hilo alilolitaja kuwa la kigaidi na kutuma salamu za pole kwa familia za waathirika pamoja na serikali ya Urusi.
Ikulu ya Marekani nayo imetuma salamu za pole kwa Urusi ikisema picha za mkasa huo ni za kuogofya na ngumu kuzitazama.
Soma pia:Watu 60 wauawa kufuatia shambulizi kwenye tamasha la muziki
Rais Xi Jinping ambae ni mshirika wa karibu wa Urusi ametuma salamu za pole na rambirambi na kusisitiza kwamba China inapinga kila aina ya ugaidi. Salamu nyingine za pole zimetolewa na viongozi wa Ujerumani, Japan, Italia, Belarus, Mexico na Venezuela.
Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umeeleza kustushwa na shambulio hilo na kusema Umoja huo unasimama na waathirika wa mkasa huo.