Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yapongezwa kimataifa
16 Januari 2025Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, ametoa wito wa kuwasilishwa kwa msaada wa haraka wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, akipongeza mpango uliofikiwa wa usitishwaji mapigano huko Gaza akisema umetokana na juhudi za Misri, Qatar na Marekani.
Wito kama huo umetolewa pia na viongozi mbalimbali wa ulimwengu ambao wamehimiza kuchukuliwa kwa hatua za ziada baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo wakisisitiza kuwepo kwa juhudi za kimataifa za kuyajenga upya maeneo yaliyoharibiwa na vita.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina, Mohammed Mustafa, amesema Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kuendelea kuishinikiza Israel kukubali kuundwa kwa dola huru la Wapalestina.
Soma pia: Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yafikiwa
Makubaliano hayo ya kihistoria ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki sita huko Gaza yanajumuisha hatua tatu ili kufanikisha kuvimaliza kabisa vita hivyo. Katika hatua ya kwanza kuwachiliwa kwa mateka 33 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas pamoja na wafungwa kadhaa wa Kipalestina.
Viongozi mbalimbali wa dunia wamepongeza makubaliano hayo wakisema yanatoa matumaini kwa raia wa pande zote ambao wamepitia mateso makubwa na kwamba yatasaidia kuendeleza juhudi za kufanikisha amani ya kudumu kati ya Israel na Palestina.
Hayo yakiarifiwa, watu 12 wameuawa hivi leo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, baada ya Israel kushambulia kwa makombora jengo la makazi. Ifahamike kuwa usitishaji huu wa mapigano huko Gaza unatarajiwa kuanza rasmi mchana wa siku ya Jumapili.