1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa ECOWAS wamtaka Keita kurejea uongozini

21 Agosti 2020

Viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wamesema watatuma ujumbe nchini Mali katika juhudi za kubatilisha mapinduzi ya kijeshi yaliofanywa nchini humo huku upinzani ukijiunga na waasi hao kupinga mwingilio wa nje.

Nigeria Ecowas-Treffen
Picha: Reuters/Str

Viongozi wa mataifa 15 wa jumuiya ya uchumi wa Afrika Magharibi ECOWAS walifanya mkutano wa dharura siku ya Alhamisi baada kuiondoa Mali katika jumuiya hiyo, kufunga mipaka yake na kusitisha shughuli za kifedha katika kujibu tukio la Jumanne la kupinduliwa kwa serikali ya rais Ibrahim Boubakar Keita. Mapinduzi hayo katika taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na mizozo ya mashambulizikutoka makundi ya kijihadi  yamelaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

Mwishoni mwa mkutano wa viongozi hao wa Ecowas, rais wa Niger Mahamadou Issoufou ambaye ni kaimu rais wa jumuiya hiyo alitoa taarifa akisema kuwa viongozi hao wanataka Keita kurejea uongozini na ujumbe utatumwa mara moja nchini Mali ambao utamjumuisha aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan. Awali duru za kidiplomasia zilisema kuwa ujumbe huo utaongozwa na viongozi wanne wa mataifa hayo.

Taarifa hiyo pia ilitoa wito wa kuongezwa kwa wanajeshi wa ECOWAS lakini haikubainsishwa wazi iwapo hatua zozote za kijeshi zitazingatiwa.

Rais Keita na waziri wake wa fedha Adoulaye Daffe waachiwa huru

Wakati huohuo ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa waakilishi wa Umoja huo wameweza kumfikia rais huyo aliyeondolewa mamlakani na viongozi wengine waliozuiliwa katika mapinduzi ya wiki hii. Ujumbe huo umeongeza kwamba hapo jana usiku ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA ulienda katika eneo la Kati katika misingi ya kutekeleza jukumu lake na kuweza kumfikia rais huyo na viongozi wengine waliokamatwa.

Hata hivyo kundi hilo la wanajeshi waasi leo limewaachia  huru rais Keita na waziri wake wa fedha Adoulaye Daffe . Keita alionekana mara ya mwisho na raia wa Mali siku ya Jumanne jioni kupitia televisheni ya kitaifa ya ORTM ambapo alitangaza kujiuzulu kwake mara moja na kuvunjuliwa mbali kwa serikali yake na bunge. Taarifa yake ilitolewa saa chache baada ya wanajeshi hao waasi kuzingira nyumba yake  na kufyatua risasi hewani kabla ya kumzuia yeye na waziri mkuu wake.

Umoja wa Mataifa na Ufaransa pia zimetoa wito wa kurejelewa kwa utaratibu wa kikatiba nchini Mali huku kukiwa na wasiwasi wa kundi la wanamgambo kukita mizizi kwa mara nyingine tena wakati huu wa msukosuko wa kisiasa na kurejesha nyuma juhudi za zaidi ya miaka saba za kuleta uthabiti katika taifa hilo. Hata hivyo msemaji wa kundi hilo la waasi Ibrahim Wague, amesema kuwa viongozi hao wapya wa kijeshi wanafanya kile wawezalo kuhakikisha kuwa hali hiyo ya uanamgambo inathibitiwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW