1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Viongozi wa EU waanza mkutano kukiwa na visiki vya Orban

14 Desemba 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametatizika mwanzoni mwa mkutano wa kilele wa siku mbili mjini Brussels juu ya kutimiza ahadi zao mbili za msingi kwa Ukraine.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor OrbanPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Miongoni mwa masuala ya kujadiliwa ni pamoja na kuiunga mkono Ukraine dhidi ya Urusi na vilevile kudumisha matumaini yake kwamba siku moja itakuwa kuwa na uwezo wa kujiunga na umoja huo tajiri.

Mkutano huo unajiri wakati muhimu katika vita vya Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi, baada ya juhudi zake kujibu mashambulizi ya Urusi kushindwa kupata mafanikio makubwa yaliyotarajiwa. Zelensky amekuwa akihimiza nchi wanachama wa EU na Marekani kuipa Ukraine misaada zaidi ya kifedha.

Hata kabla ya mkutano kuanza, maafisa na wanadiplomasia walisema walikuwa wakijiandaa kwa mfululizo wa mazungumzo magumu ambayo yanaweza kwenda hadi Ijumaa usiku au hata wikendi.

Ikiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wataruhusu kuanzishwa kwa mazungumzo ya uanachama wa Ukraine pamoja na mpango wa msaada kwa miaka minne, basi Kyiv itaweza kudai kupata ushindi wa siasa za kijiografia. Endapo watakosa kukubaliana basi, kwa Urusi, hiyo itakuwa ishara ya kuporomoka kwa uungwaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ametilia msisitizo hoja ya kuisaidia Ukraine:

"Lakini sote tunajua kwamba kushindwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin hakuwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ushindi wa Ukraine. Wakati vita vinaendelea, lazima tuthibitishe maana au haja ya kuunga mkono Ukraine bila kujali vita vitachukua muda mrefu kiasi gani. Ukraine haipigani tu dhidi ya mvamizi, lakini vilevile kwa Ulaya; na kujiunga na familia yetu itakuwa ushindi wa mwisho wa Ukraine. Na kwa hili, tuna jukumu muhimu la kutekeleza."

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky asema Hungary haina sababu yoyote ya kuzuia mazungumzo ya uanachama wake katika Umoja wa Ulaya.Picha: AFP/Getty Images

Visiki vya Orban

Viongozi wote wa wa nchi 27 za umoja huo isipokuwa waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban wameunga mkono kuanzishwa kwa mazungumzo ya uanachama wa Ukraine. Kisiki ni kwamba uamuzi kama huo unahitaji kuungwa mkono na wanachama wote. Hungary ambayo inajenga uhusiano wa karibu na Urusi inasisitiza kuwa Ukraine haiko tayari kwa hatua kama hiyo.

Zelensky ateta na Orban uanachama wa Ukraine Umoja wa Ulaya

Mnamo mkesha wa mkutano huu wa kilele, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema nchi yake imetekeleza ipasavyo mageuzi ya kisiasa ili kupata ridhaa na kuitaka Umoja wa Ulaya kuheshimu ahadi zake.

Kupitia mtandao wake wa kijamii aliandika "Ninategemea viongozi wa Umoja wa Ulaya kutambua juhudi za Ukraine na kuchukua hatua hii ya kihistoria, Ukraine imetimiza sehemu yake na kuthibitisha kwamba inaweza kupata matokeo makubwa licha ya changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa”.

Orban pia anapinga pendekezo la tume ya umoja huo kuipa Ukraine euro bilioni 50 kama misaada na mikopo ya kuwezesha serikali hiyo kuendesha shughuli zake.

Hungary: Je Orban ana tatizo gani na Ukraine?

Hiyo ikiwa ni sehemu ya marekebisho mapana ya bajeti ya Umoja wa Ulaya. Marekebisho kama hayo pia yanahitaji kuungwa mkono nan chi zote wanachama.

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ni miongoni mwa wanaoongoza juhudi za kidiplomasia na Viktor Orban.Picha: Kay Nietfeld/AP/dpa/picture alliance

Juhudi za kidiplomasia za Scholz na Macron

Kama ishara ya juhudi kubwa za kidiplomasia katika suala hili, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela Olaf wa Ujerumani Scholz walipangwa kukutana asubuhi na Orban pembeni  kabla ya mkutano wa kilele, pamoja na mkuu wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen na Mkuu wa Baraza Charles Michel.

Katika kutetea msimamo wake, Orban ametaja ufisadi nchini Ukraine na masuala mengine.

Lakini maafisa wa umoja huo na wanadiplomasia wanashuku kwamba anatumia suala hilo kama chambo akitumai kupata fedha za Hungary ambazo Umoja wa Ulaya umezuia kufuatia wasiwasi juu ya utawala wa sheria wa taifa hilo.

Mnamo Jumatano, Tume ya Ulaya, iliirudishia Hungary uwezo wa kupata hadi euro bilioni 10.2 kwa miradi ya kiuchumi baada ya kubaini kuwa nchi hiyo imetimiza masharti ya uhuru wa mahakama yake.

Vyanzo: RTRE, APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW