Viongozi wa EU waendelea na mkutano wao uliojaa "hamaki"
18 Julai 2020Majadiliano hayo yanatuwama zaidi katika kutaka kuzisaidia zile nchi zilizoathirika zaidi na kusambaa kwa virusi vya corona. Katika mkutano huo hali ya wasi wasi iko juu miongoni mwa viongozi ambao wamefikia hatua ya kuchoka baada ya miezi kadhaa ya kupambana na janga la virusi vya corona katika nchi zao.
Siku nzima na usiku za majadiliano ya viongozi 27 siku ya Ijumaa yaliongeza tu hali ya kutoridhika kuhusiana na vipi fedha hizo nyingi zitatumika na masharti gani yanapaswa kuwekwa.
Hali "ilikuwa hamaki" wakati mazungumzo hayo yakiendelea , waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alisema baada ya mazungumzo ya muda mrefu siku ya Ijumaa. "Hii itachukua muda kidogo, nafikiri."
Halmashauri ya utendaji ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza mfuko wa euro bilioni 750, kwa sehemu fulani chini ya mfumo wa kawaida wa kukopa, utakaowekwa kama mkopo na misaada kwa zile nchi ambazo zitakuwa na uhitaji mkubwa. Hii inakuja juu ya bajeti ya Umoja wa Ulaya ya miaka saba yenye thamani ya euro trilioni 1 ambayo viongozi walikuwa wakipambana huku ugonjwa wa COVID-19 ukishambulia bara lao.
Mapendekezo mapya
Mkutano huo uliahirishwa wakati wa chakula cha mchana leo Jumamosi(18.07.2020) ili kila ujumbe uweza kujadili mapendekezo mapya kutoka kwa mwenyeji wa mkutano huo Charles Michel, kwa mujibu wa mwanadiplomasia wa Ulaya.
Mapendekezo hayo mapya yanapunguza kiwango cha misaada ya moja kwa moja katika mfuko wa uokozi na kupandisha kiwango cha mikopo ambacho kitahitajika kulipwa , katika muda ambao kundi la mataifa pinzani kwa mpango huo yakiongozwa na Uholanzi yataridhia, amesema mwanadiplomasia huyo.
Lakini ufuatiliaji wa fedha za uokozi bado unabaki kuwa kikwazo kikubwa, mwanadiplomasia huyo alisema. Michel alipendekeza hatua ambayo haitafika kuruhusu nchi yoyote kutumia kura ya turufu juu ya vipi serikali zinaweza kutumia fedha hizo.
Mwanadiplomasia mwingine ameyaeleza mapendekezo mapya ya Michel kama hatua tu ya kwanza katika kile ambacho kinaweza kuwa safari ndefu kuelekea makubaliano. Wanadiplomasia wote hao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwasababu hawakuidhinishwa kujadili masuala hayo yanayojadiliwa kwa faragha kwa umma.